1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi uchaguzi wa Msumbiji watilia shaka mchakato mzima

12 Oktoba 2024

Waangalizi wa kimataifa kwenye uchaguzi wa Msumbiji wameelezea kuwepo kwa matukio kadhaa ya udanganyifu, huku vyama vya upinzani vikisema uchaguzi huo wa Jumatano uliofanyika katika hali ya amani, ulijaa wizi.

Daniel Chapo
Mgombea urais wa Msumbiji kupitia chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo.Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP/Getty Images

Katika taarifa yao ya hapo jana, waangalizi wa Umoja wa Ulaya walisema walishuhudia mabunda ya karatasi za kura zikiwa zimeshapigwa kwenye maeneo kumi tafauti.

Wasiwasi wa udanganyifu ulielezewa pia na Taasisi ya IRI ya Marekani, ambayo waangalizi wake wamekosowa jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika.

Soma zaidi: Msumbiji yaanza kuhesabu kura

Kwa mujibu wa waangalizi hao, chama tawala cha Frelimo kilitumia vibaya rasilimali za nchi, wakiwemo wafanyakazi na vyombo vya usafiri vya umma, wakati wa kampeni. Kwenye majimbo yenye wafuasi wengi wa chama hicho, usajili wa wapigakura ulivuuka asilimia 100.

Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola wamezitaka mamlaka husika kuyashughulikia madai yote ya udanganyifu.

Ingawa matokeo rasmi hayatazamiwi kupatikana kabla ya wiki mbili zijazo, mgombea wa Frelimo, Daniel Chapo, anatarajiwa kushinda kwa wingi wa kura.