Waangalizi wa Arab League watakiwa kuondoka Syria
2 Januari 2012Vikosi vya ulinzi vya Rais Bashar al-Assad, vimekuwa vikidhibiti vikali maandamano makubwa mbele ya macho ya waangalizi wa nchi za kiarabu na kudaiwa kuuwa kiasi ya watu 286, tangu Desemba 23, siku moja kabla ya ujumbe wa waangalizi kutoka nchi za kiarabu kuwasili nchini Syria.
Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu ambao wamekuwa wakifuatilia mikasa inayotokea nchini humo wamedai watu wanane waliuwawa kwa kupigwa risasi wakati vikosi vya ulinzi vilipowafyatulia risasi waandamanaji katika kiunga kimoja cha Damascus, Daria.
Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, chombo lenye wabunge 88 linye kuunganisha wawakilishi kutoka nchi za jumuiya hiyo limesema vurugu zinaendelea kuathiri watu wengi.
Mwenyekiti wake, Ali al-Salem al-Dekbas alisema kutokea kwa jambo hilo kunaongoza hasira kwa jamii ya Kiarabu na inakwenda kinyume na madhumuni ya kutuma ujumbe wa kutafuta ukweli nchini Syria.
Kiongozi huyo aliendelea kwa kusema vitendo hivyo ni sawa na kutoa ridhaa ya kwa utawala wa nchi hiyo kuwafanyia maovu watu mbele ya masikio na macho ya Arab League.
Wapinzani wa Assad, waliukaraibisha ujumbe wa nchi za Kiarabu nchi humo ikionekana kama nafasi ya nadra sana kwa watu wa nje kuingia kushuhudia juu ya hali ya mambo yalivyo nchini humo. Lakini pia walikuwa na matumaini duni kama ujumbe huo ungeweza kufanikisha kuufikisha kikomo ukandamziaji ambao Umoja wa Mataifa unakadiria zaidi ya watu 5,000 kuuwawa tangu Machi.
Waangalizi hao nchini Syria wanafuatilia utekelezaji wa mpango wa amani wa Arab League ambao unamtaka rais Assad kuondoa majeshi mitaani, kuwachia uhuru watu aliowatia kizuizini pamoja na kufungua milango ya mazungumzo na wapinzani.
Awali Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil Elaraby alisema itawachukua wiki moja tu kubaini kama Assad anatakeleza yale aliyoahidi.
Mpinzani, mwingine alisdema Rima Fleihan, kutoka Baraza la Kitaifa la Syria SNC alisema uwepo wa waangalizi hakujaathiri tabia ya utawala wa nchi hiyo ya kuendeleza mauwaji.
Waangalizi wa hao pamoja na maeneo mengine walitembelea mji wa Deraa eneo la mwanzo la vuguvugu la kumpinga Assad lilipoanza na kufika nyumbani kwa Sheikh Ahmad Hayasneh, imam mkuu wa msikiti wa Omari.
Msikiti huo ndipo kulipoanza maandamano ya awali ya kuupinga utawala wa Assad ingawa pia haijawa wazi kama kiongozi huyo alipatikana kwa kuwa inadaiwa kwamba amewekwa katika kifungo cha nyumbani kwa zaidi ya miezi mitano sasa.
Mwandishi: Sudi Mnette/RTR
Mhariri: Mohammed Khelef