Waangalizi wa EAC Kenya na Kinagaubaga
19 Februari 2013Jumuiya ya Afrika Mashariki wiki hii imetuma ujumbe wake wa waangalizi ukiongozwa na aliyekuwa spika wa bunge la Afrika Mashariki Abdurahman Kinana anayetokea nchini Tanzania. Itakumbukwa kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2007 katika taifa hilo la Afrika Mashariki baadhi ya viongozi wa kisiasa walivitupia lawama vyombo vya waangalizi wa kigeni kwa kudai vinatoa ripoti ambazo hazina ukweli vilipodai kwamba kulikuwepo udanganyifu katika uchaguzi huo ambao matokeo yake yalitangazwa kwa njia za utata ghafla na aliyekuwa wakati huo mkuu wa tume ya uchaguzi Samuel Kivuitu baada ya kuzuka vurugu katika ukumbi yalikokuwa yakitangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo.
Tume ya waangalizi ya Umoja wa Ulaya ilisema uchaguzi huo wa mwaka 2007 ulikosa kuzingatia sheria muhimu za Kimataifa na zile za kikanda za uchaguzi wa kidemokrasia, kwa mujibu wa tume hiyo utaratibu mzima wa kuhesabu na kutangaza matokeo ulikumbwa na hali ya kukosekana uwazi jambo ambalo lilisababisha kucheleweshwa kwa matokeo ya urais na hatimaye wananchi wakapoteza subira hali iliyozusha vurugu zilizogeuka kuwa vita kamili vya kikabila.
Je waangalizi wa uchaguzi kutoka nje watakuwa na mchango gani na wamejiandaa vipi katika kuepusha lawama.Katika Kinaga Ubaga Saumu Mwasimba amezungumza na kiongozi wa kundi la waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki AbdulRahman Kinana na kwanza anataka kujua maandalizi yeo yamefikia wapi katika kuusimamia uchaguzi wa Kenya Marchi nne.
Kusikiliza mahojiano hayo bonyeza alama ya kusikiliza masikioni hapo nchini
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo