1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yasema rais wa zamani wa Kongo yuko Goma

Saleh Mwanamilongo
26 Mei 2025

Kundi la waasi wa M23 huko mashariki mwa Kongo limesema kwamba rais wa zamani wa Kongo Joseph Kabila amewasili katika mji wa Goma unaodhibitiwa na waasi hao.

Joseph Kabila amewasili Goma siku chache baada ya serikali kuondoa kinga ya Kabila kutoshtakiwa, ili kufungua njia ya kumshtaki kwa uhaini
Joseph Kabila amewasili Goma siku chache baada ya serikali kuondoa kinga ya Kabila kutoshtakiwa, ili kufungua njia ya kumshtaki kwa uhainiPicha: Reuters/K. Katombe

Kiongozi wa muungano wa kisiasa na kijeshi wa waasi wa AFC/M23, Corneille Nangaa ametangaza kuwa Joseph Kabila amewasili katika mji wa Goma. Kwenye ujumbe kupitia ukarasa wake wa X, Nangaa amesema kwa pamoja na Kabila wanadhamiria kukomesha kile alichokiita kuwa ni "udikteta na migawanyiko" nchini Kongo.

Kurejea kwa Kabila nchini Kongo kumethibitishwa pia na watu wa karibu yake. Kikaya Bin Karubi aliyekuwa mshauri wake wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia ameiambia DW kwamba Kabila aliwasili usiku wa kuamkia Jumatatu, lakini hakufahamaisha ajenda na muda ambao kiongozi huyo wa zamani wa Kongo atasalia hapo Goma.

Duru nyingine ya karibu na Joseph Kabila imesema ziara hiyo niyamshikamano na raia wa Kivu walioathirika na vita na kwamba anampango wa kurejesha amani ambao atawawakilisha pia kwa waasi wa AFC/M23.

Ijumaa iliopita, Kabila alimkosoa Rais Félix Tshisekedi kwa kile alichokiita uongozi mbaya, akisema kuwa umelitumbukiza taifa katika mgogoro wa "kimuundo" na kuifanya Kongo kuwa kichekesho mbele ya jamii ya kimataifa.

Katika hotuba aliyoitoa baada ya kuondolewa kwa kinga yake ya kisheria, Kabila alitetea utawala wake, akisisitiza kuwa Tshisekedi ameharibu misingi imara aliyoacha baada ya miaka 18 ya urais.

"Rais Kabila amepitwa na wakati"

Wafausi wa chama tawala UDPS nmchini Kongo wakosoa hotuba ya KabilaPicha: Paul Lorgerie/DW

Mjini Kinshasa, hotuba ya Joseph Kabila na ziara yake huko Goma vimechukuliwa kama kitendo cha usalati wa taifa na kwa demokrasia. Akihojiwa na televisheni ya taifa, msemaji wa serikali ya Kongo, Patrick Muyaya amesema kuwa Kabila amepitwa na wakati na alitakiwa kunyamaza.

"Tumeona maoni ya Wakongo baada ya hotuba ya Kabila. Maoni ya Wakongo waliowengi kwenye mitandao ya kijamii ni ishara tosha kuhusu wanachofikiria : kwa hakika, Rais Kabila amepitwa na wakati, ambaye hana jambo jipya la kupendekeza kwa ajili ya mustakbali wa taifa. Kwa upande wetu, sisi tunajikita katika kutatua matatizo ambayo yeye Kabila hakuweza kuyatatua wakati alipokuwa madarakani", alisema Muyaya.

Akiwahutubia wafuasi wao kwenye makao makuu ya chama jijini Kinshasa, Augustin Kabuya, katibu mkuu wa chama tawala UDPS, alimtuhumu Kabila kwa kudhoofisha jeshi la Kongo na kuchangia uingiliaji kati wa Rwanda wakati alipokuwa rais.

Kabuya amesema kiongozi halisi wa waasi wa M23 na mtu aliyechangia kufilisika kwa taifa la Kongo ni Joseph Kabila katika uongozi wake wa miaka 18 wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali za madini.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW