Waasi wa ADF wawaua watu 60 Kivu Kaskazini
9 Septemba 2025
Hili ni tukio jingine la umwagaji damu katika eneo ambalo mashambulizi yanayohusishwa na ADF yamekuwa yakijirudia kwa miaka mingi.
Mashambulio hayo yalitokea muda mfupi baada ya saa tatu usiku, ambapo wakazi waliokusanyika kwa maombolezo walivamiwa ghafla na waasi. Kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo, zaidi ya watu 60 wameuawa, lakini mashuhuda na manusura wanasema idadi ya vifo inaweza kuzidi mia moja, wengi wao wakiwa wamechinjwa kwa mapanga.
Kanali Alain Kiwewa, ni kiongozi wa wilaya ya Lubero anasema Sekta ya Bapere imejaa migodi ya dhahabu ambayo huenda ikawa sababu ya mashambulizi.
"Tunakadiria kuwa idadi ya vifo imefikia karibu watu sitini hadi sasa, lakini bado hatujathibitisha rasmi kwa sababu timu zetu hazijafika kuhesabu waliokatwa shingo. Tukio lilitokea jana kati ya saa tatu na saa nne usiku. Sekta ya Bapere imejaa migodi ya dhahabu na mashamba ya kahawa, ambazo huenda zikawa sababu ya mashambulizi haya," alisema Alain Kiwewa.
Mauaji haya mapya yamesababisha maelfu ya wakazi kukimbia makazi yao. Familia nyingi zimeelekea Njiapanda, Butembo na maeneo mengine yanayochukuliwa kuwa salama zaidi.
Kwa mujibu wa Claude Musavuli, mtetezi wa haki za binadamu, kijiji kizima kimefutwa ramani bila hata upinzani wowote kutoka vyombo vya usalama. Anasema udhaifu wa Jeshi la Congo (FARDC) unadhoofisha pia ushirikiano wao na wanajeshi wa Uganda (UPDF).
"Tuna matatizo ndani ya muungano wa FARDC-UPDF kwa sababu kuna wanajeshi wengi wa FARDC ambao wamehudumu hapa kwa miaka mingi na wamekuwa kama wenyeji. Ni lazima tubadilishwe. Lakini tatizo jingine ni mlolongo wao mrefu wa uongozi. Wakati muungano unasubiri maamuzi ya mnyororo huo, ADF wanazidi kuimarika. Tayari wameua zaidi ya raia kwa mamilioni, na wengine wamezikwa bila kujulikana. Nimesafiri vijijini na nimeona mifupa mingi ya binadamu."
ADF ni miongoni mwa makundi kadhaa ya waasi yanayowania ardhi na rasilimali mashariki mwa Congo, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini. Jeshi la Congo likishirikiana na Uganda linasema limeimarisha operesheni dhidi ya kundi hilo katika wiki za hivi karibuni.
Mwezi uliopita pekee, ADF waliua zaidi ya raia 50 katika mashambulizi mbalimbali, huku shambulio jingine la mwezi Julai likiua watu 38 katika kanisa moja.