Waasi wa Azawad watangaza vita na utawala wa kijeshi Mali
12 Septemba 2023Kauli hii inajiri huku shirika la ndege la Sky Mali, likitangaza kusitisha safari zake kuelekea miji ya kaskazini ya Timbuktu na Gao baada ya uwanja wa ndege wa Timbuktu kushambuliwa kwa makombora.
Soma pia: Shambulizi la kujitoa mhanga latokea dhidi ya kambi ya jeshi Mali baada ya 64 kuuawa
Mali imeshuhudia kuzuka tena kwa hali ya wasiwasi katika wiki za hivi karibuni,baada ya kuondoka kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka nchini humo.
Muungano wa makundi wa CMA ulio na wafuasi wengi kutoka kabila la Watuareg wanaotaka kujitawala au kujitenga na Mali, kupitia taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii waasi hao wametoa wito kwa wakaazi wote wa eneo la kaskazini la Azawad "kujitolea katika kuchangia juhudi za vita."
Katika taarifa hiyo CMA ilisema madhumuni yake ni "kulinda nchi na hivyo kurejesha udhibiti wa eneo lote". Hii ikiwa hati ya hati ya kwanza iliyotiwa saini na kundi linalojiita "Jeshi la Taifa la Azawad".
Soma pia: Kundi la JNIM ladai kuishambulia kambi ya jeshi Mali
Aidha hati hiyo pia ilitoa wito kwa raia kukaa mbali na "magaidi wa Wagner", hii ni kutokana na kwamba Jeshi la Mali linaaminika kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanamgambo wa Urusi Wagner.
Shirika la ndege lasitisha huduma
Shirika la ndege la Mali Sky, limetangaza kusitisha safari za ndege kuelekea miji ya kaskazini ya Timbuktu na Gao baada ya makombora kutua karibu na uwanja wa ndege wa Timbuktu.
Kulingana na afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa aleyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, Makombora matatu yalipiga karibu na eneo la uwanja wa ndege, huku mawili yakipiga kambi ya misheni ya Umoja wa Mataifa Jumatatu asubuhi. Hata hivyo hakukuwa na majeruhi wowote.
Rais wa Chama cha Raia wa Timbuktu huko Bamako, Sandy Haidara, alisema shambulio hilo lilifanyika wakati Sky Mali ikikagua abiria.
Timbuktu tangu mwezi Agosti imekuwa chini ya kizuizi kilichowekwa na kundi la wanamgambo wenye itikadi za kiisilamu la GSIM lilolo na mafungamano na Al-Qaeda.
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Dennis Francis amewataka wajumbe wa Baraza la Usalama kujitolea tena kwa mazungumzo kuelekea amani na maridhiano nchini Mali.
"Baraza la Usalama lina jukumu la msingi la kudumisha amani na usalama wa kimataifa. Ninawaomba wanachama wake kujitolea tena kwa mazungumzo ili kuendelea kufanyia kazi malengo haya kuelekea amani na maridhiano nchini Mali. Hapa katika Mkutano Mkuu, mpango wa kura ya turufu unatoa fursa ya kuwa suluhu katika wakati huu wa mzozo.” alisema Dennis Francis.
Kaskazini mwa Malikumekuwa chini ya shinikizo la usalama kwa wiki kadhaa, na kuibua hofu ya kuongezeka kwa mgogo mpya kati ya makundi mbalimbali yenye silaha yanayowania udhibiti wa kikanda.