Waasi wa Houthi waelekea Oman kwa matibabu
3 Desemba 2018Kuondolewa waasi hao mjini Sanaa kupitia ndege ndogo ya Umoja wa Mataifa kunafungua njia ya majadiliano yaliyokwama ya kutafuta amani nchini Yemen huku viongozi wa dunia wakishinikiza kumalizika mapigano yaliyodumu miaka minne yalioisukuma Yemen katika hatari ya kukabiliwa na njaa.
Msemaji wa muungano huo, Turki al-Maliki, amesema ndege hiyo itawabeba waasi hao 50 pamoja na madaktari watatu wa Yemen kutoka Sanaa hadi katika mji mkuu wa Oman, Muscat. Hatma ya waasi walioumia lilikuwa moja ya mambo yaliokwamisha kuanza kwa mazungumzo ya amani yaliyofeli mwezi Septemba.
Umoja wa Mataifa unajaribu kuwaweka pamoja waasi wa Houthi nan a serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia kukaachini katika meza ya mazungumzo mwezi huu.
Huku hayo yakiarifiwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Yemen Martin Griffiths amewasili mjini Sanaa hii leo, kwa mazungumzo na waasi kuelekea jaribio jingine la mazungumzo ya amani kuleta pande zinazohasimiana katika meza ya mazungumzo.
Ziara yake inakuja wakati kukiwa na shinikizo la kufungua uwanja wa ndege unaoshikiliwa na waasi iliofungwa kwa zaidi ya miaka mitatu kufuatia mashambulizi ya angani yaliofanywa na muungano wa Saudi Arabia. Umoja wa Mataifa umesema kufunguliwa kwa uwanja wa ndege huo ni kipaumbele katika azungumzo ya kurejesha amani ya Yemen.
Iran yaunga mkono juhudi za kurejesha amani Yemen
Wakati huo huo Iran imeunga mkono juhudi za mazungumzo yamani zinazofanywa na Umoja wa Mataifa ikitoa wito wa kumalizika kwa mateso nchini Yemen.
Katika taarifa yake waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Javad Zarif, amesema wapenda vita bado hawajapata mafanikio yoyote ya kisiasa katika miaka minne ya mapigano na uchokozi uliofanywa kwa watu wa Yemen.
Wizara ya kigeni imesema viongozi wa dunia wanapaswa kushinikiza wasafirishaji wa silaha kwa makundi ya kihalifu kuunga mkono mazungumzo ya amani na kuwawachia wayemeni wenyewe kuamua mambo yao bila ya kuingiliwa na mataifa ya nje.
Mataifa ya Guba ya kiarabu pamoja na Marekani zinaishutumu Iran kwa kuwaungamkono waasi wa Houthi na kuliona hili kama kisingizio cha kuendelea na kampeni yake ya kijeshi ilioanzisha kuanzia mwezi Machi mwaka 2015.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef