Waasi wa Kihouthi waenda Sweden kwa mazungumzo ya amani
4 Desemba 2018Safari ya wapiganaji hao wa Kihuthi inafuatia makubaliano ya kubadilishana wafungwa pamoja na kuondolewa kwa waasi 50 waliojeruhiwa kwenda kupata matibabu nchini Oman katika hatua muhimu ya kuimarisha juhudi hizo za amani.
Ujumbe huo umeongozana na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths , kimesema chanzo katika uwanja wa ndege. Msemaji wa waasi Mohammed Abdelsalam amethibitisha kuondoka kwao katika maelezo aliyoyatoa katika ukurasa wa Twitter, akisema Wahuthi hao "hawataacha juhudi za kuyafanya mazungumzo hayo ya mafanikio ili kurejesha amani na kumaliza matumizi ya nguvu na uchokozi".
Wakati huo huo aliwataka wapiganaji wa waasi kuendelea kubakia waangalifu dhidi ya juhudi zozote zitakazo chochea hatua za kijeshi".
Licha ya kwamba hakuna tarehe kamili iliyotangazwa kwa ajili ya kuanza mazungumzo hayo, duru za serikali ya Yemen zinasema mazungumzo hayo yanaweza kuanza siku ya Alhamis.
Waziri wa habari na msemaji wa Wahothi mjini Sanaa Daifallah Al-Shami hapo kabla alisema kwamba pamoja na kuelekea huko nchini Sweden lakini hawajapata mualiko rasmi.
"Hadi sasa hatujapata mwaliko wowote moja kwa moja kutoka Umoja wa mataifa kwa ajili ya mazungumzo hayo nchini Sweden. Kutokana na juhudi za Umoja wa mataifa na mjumbe wake maalum , hatuwezi kuona mwelekeo wa wazi kwa ajili ya mazungumzo hayo."
Makubaliano ya kubadilishana mamia ya wafungwa yalikaribishwa na kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu, shirika ambalo litaangalia mabadilishano hayo baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo yaliyopangwa ya amani nchini Sweden.
Makubaliano hayo yalifikiwa kwa upatanishi wa Griffiths, ambaye alikuwa katika mji mkuu unaoshikiliwa na waasi wa Sanaa kwa ajili ya mikutano ambayo tayari ilikwisha tiwa shime na kuondolewa kwa wapiganaji ambao walikuwa wamejeruhiwa, sharti moja muhimu la waasi kwa ajili ya mazungumzo hayo.
Juhudi za awali za Umoja wa mataifa kufanya upatanishi na kuwaleta pamoja Wahuthi na serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia katika meza ya majadiliano zilivunjika nchini Uswisi mwezi Septemba.
Umoja wa Falme za Kiarabu , nchi nyingine muhimu inayounga mkono serikali ya nchi hiyo, imesema mazungumzo hayo yaliyopangwa yanatoa fursa muhimu , ya kumaliza karibu miaka minne ya vita.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Khelef