Waasi wa M23 waelekea Goma
1 Agosti 2012Umoja wa Mataifa umefanya mkutano wa dharura hapo Jumanne (tarehe 31 Julai) juu ya kusonga mbele kwa waasi wa M23 kuelekea makao makuu ya mkoa huo, Goma. Baraza la Usalama pia linajadiliana kutoa taarifa ya kuwaonya waasi wanaosemekana kuungwa mkono na Rwanda.
Kwa mujibu wa wanadiplomasia katika Umoja wa Mataifa, Mjumbe Maalum wa Umoja huo kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Roger Meece, aliwapa wajumbe 15 wanachama wa Baraza la Usalama taarifa fupi inayoonya juu ya kitisho kipya kwa serikali ya nchi hiyo yenye utajiri wa rasilimali.
"Vikosi vya serikali vinaishiwa na silaha na wanaviacha vijiji mikononi mwa M23. Hii inazusha masuala kuhusu uwezo wa jeshi la serikali, kwani jeshi hilo limepata madhara makubwa sana." Alisema Meece kwa mujibu wa wanadiplomasia hao.
M23 waelekea Goma
Waasi hao wanaoongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda anayetakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, walijitenga na jeshi la serikali mwezi Aprili na kuanzisha vuguvugu la uasi dhidi ya serikali. Vikosi vyao vinavyoaminika kuwa na silaha za kisasa, sasa vinakaribia mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini, Goma, katika eneo linalopakana na Uganda na Rwanda.
M23 wamesogeza makao yao makuu katika mpaka unaoelekea Goma, wakiichukua miji na vijiji kadhaa bila ya hata kukabiliwa na upinzani wowote, kwa mujibu wa wanadiplomasia wanaonukuu taarifa kutoka eneo hilo.
Kundi la waasi wa M23 linaundwa na wapiganaji wa Kitutsi walioingizwa jeshini mwaka 2009, lakini wakaasi mwezi Aprili mwaka huu kwa madai ya mishahara na hali duni za maisha. Msemaji wa waasi hao, Kanali Innocent Kayima, amesema wanakusudia kuuchukua mji wa Goma.
MONUSCO kuwalinda raia
Kikosi cha kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Congo (MONUSCO), mara kadhaa kimetumia helikopta zake kulisaidia jeshi la serikali, lakini sasa inaonekana kama kwamba jeshi hilo halisaidii tena.
"MONUSCO inawalinda raia na imekuwa ikipeleka vikosi vyake kila sehemu kwa ajili ya lengo hilo," alisema naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Eduardo del Buey, alipoulizwa ikiwa vikosi zaidi vitapelekwa kwenye maeneo yaliyotwaliwa na M23. Hata hivyo, hakutoa undani wa operesheni ya MONUSCO kwa sababu za kiusalama.
MONUSCO ndicho kikosi kikubwa kabisa ya operesheni ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kikiwa na kiasi wanajeshi na polisi 19,000 waliotawanyika nchi hiyo kubwa kabisa katika eneo la Mashariki na Kati ya Afrika. Hata hivyo, wakosoaji wanasema kwamba kikosi hicho hakina uwezo wala idhini ya kupambana na waasi wa M23.
Serikali ya Congo yaendelea kuishutumu Rwanda
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaituhumu Rwanda kwa kuwafadhili waasi wa M23. Serikali hiyo imesema kwamba haitazungumza na waasi wanaochochea ghasia, ingawa msemaji wake, Lambert Mende, alisema kwamba majadiliano yanawezekana kufanyika na Rwanda.
Kauli ya Mende ya hapo Jumatatu (tarehe 30 Julai) inatafautiana na gavana wa Kivu ya Kaskazini ambaye alisema kwamba ni lazima serikali iupitie tena mkataba wake wa mwaka 2009 uliowaingiza waasi jeshini kuona kuwa inautekeleza.
Jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa pia linasema kwamba vifaa na wapiganaji wa kundi hilo wametolewa na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Rwanda. Lakini serikali ya Rwanda imekanusha vikali tuhuma hizo.
"M23 wanaonekana wana silaha nzuri zaidi kuliko jeshi la serikali na idadi ya wapiganaji imekuwa ikiongezeka katika siku za hivi karibuni," alisema afisa mmoja wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo yake na shirika la habari la AFP.
Zaidi ya watu 470,000 wameyakimbia makaazi yao katika eneo la mashariki ya Congo tangu mwezi Aprili huku 50,000 wakielekea katika nchi za Uganda na Rwanda.
Umoja wa Mataifa unasema umepokea ripoti za unyanyasaji, mauaji ya makusudi dhidi ya raia, ubakaji na mateso.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Miraji Othman