Waasi wa M23 wajaribu kuushambulia mji wa Sake
8 Januari 2025Mapigano hayo karibu na mji wa Sake yalitokea siku ya Jumanne Januari 7 asubuhi kwenye mlima Kihuli na Kimoka kijiji kilichoko kilomita 5 kutoka mji huo wa kimkakati.
Soma ripoti hii: Zaidi ya watu 100,000 wakimbia makaazi yao chini ya wiki moja mashariki mwa Kongo
Taarifa zinasema kuwa wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaosaidiwa na wanamgambo wazalendo, walizishambulia kwa mizinga ngome za waasi wa M23 waliojaribu kuushambulia mji wa sake kilomita 27 magharibi mwa mji wa Goma.
Wakati mapigano yalikuwa yakiendelea, mabomu yalirushwa maeneo yanayokaliwa na waasi na kuangukia katikati mwa mji wa Sake na kuwauwa watu wananne wakiwemo watoto na wanawake,kama anavyo eleza Batachoka Douglas raia aliyeshuhudia tukio hilo baya.
"Mapigano yalianzia huko Kihuli ambapo wazalendo walipambana na M23 ,majira ya sambili unusu waasi wa M23 wakatupa bomu katika mji wa Sake na kuwauwa watu watatu na mmoja kujeruhiwa ambaye alifariki pia saa chache akiwa hospitalini huko CEBCA Ndosho ".
Upande mwingine katika wilaya hiyo ya Masisi, jeshi tiifu kwa serikali ya kongo, FARDC na vikundi vya wenyeji wenye silaha, vilichukua udhibiti wa vijiji vya Ruzirantaka, Kabingo, Kadahangwa na Kashovu kilomita nne kutoka mji mwingine unaokaliwa na M23 wa Ngungu, kama anavyobainisha raia huyu.
Soma: M23 wakaribia kuudhibiti mji muhimu mashariki mwa DRC
"Ndio wanajeshi wa serikali wanaukaribia mji wa Ngungu na muda huu wapo kwenye kilomita 2 na mji. Mapigano yalipamba moto tangu juzi na hadi sasa yanaendelea. Jeshi la serikali limedhibiti vijiji vya Kamatale, Ruzirantaka , Rwangara na sasa kijiji cha Katahandwa ni kilomita 2 tu na mji wa Ngungu ".
Hadi kufikia siku ya Jumatano, hali imesalia kuwa ya wasiwasi katika maeneo kadhaa wilayani Masisi, ambamo jeshi la Kongo linalosaidiwa na vijana wazalendo limezidisha mashambulizi dhidi ya vijiji vilivyochukuliwa na waasi wiki moja iliyopita.
Wakazi wa vijiji vya Kaniro, Kinigi na Kahongole karibu na mji mkuu wa wilaya hiyo Masisi ,wameshuhudia milio ya mizinga inayowafanya baadhi kukwama msituni.Marekani yailaani M23 kwa kuvunja usitishaji mapigano
Mungu Akonkwa Safari ni mwanasiasa toka jopo la vyama vinavyo muunga mkono Rais Felix Tshisekedi.
"Huu ndio muda kwa wale wanasiasa wanaojiita ma profesa na wenye ujuzi mwingi katika siasa ni muda wakuliokoa taifa sababu laelekea kuanguka. viongozi wote tafadhali , muweke fikra zenu pamoja ili kutafuta amani."
Mapigano hayo, yamezidi baada ya M23 kuchukua Masisi, mji mkuu wa wilaya hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.