1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Waasi wa M23 wakaribia jimbo lenye utajiri wa madini Kongo

11 Novemba 2024

Umoja wa Mataifa umesema ushawishi wa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika sehemu za mashariki mwa Kongo sasa umeongezeka kwa asilimia 70 zaidi kuliko mwaka uliopita.

Waasi wa M23, Kongo
Mashambulizi ya M23 yananuia kuchukua udhibiti wa madini muhimu ya mashariki ya KongoPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Katika muda wa miaka mitatu, Vuguvugu la Machi 23 au M23 limefanikiwa kukalia sehemu kubwa za mkoa wa Kivu Kaskazini uliyoko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wameweza kupanua ushawishi wao katika maeneo matano kati ya sita ya jimbo hilo, Rutshuru, Nyiragongo, Beni, Masisi na Walikale.

Soma pia: M23 waukamata tena mji wa Kalembe mashariki ya Kongo

Kulingana na Umoja wa Mataifa, eneo la ushawishi wa M23 ni kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa na linawakilisha ongezeko la asilimia 70 ikilinganishwa na Novemba 2023. Hali katika wilaya ya Walikale, hasa kijiji cha Pinga, bado haiko wazi kutokana na mapigano kati ya M23 na jeshi la Kongo (FARDC), likisaidiwa na wanamgambo wa kundi linalojiita Wazalendo.

Soma pia: Msemaji wa jeshi la Kongo asema jeshi limeurejesha mji wa kalemba kwenye udhibiti.

Mashambulizi ya M23 yanafuata mantiki ya wazi: wanataka kudhibiti madini ya eneo hilo - hasa dhahabu, koltani, kobalti, na almasi. Baada ya kuchukua sehemu za maeneo ya Rutshuru na Masisi, waasi hao wanakwenda kuelekea Walikale, ambao unajulikana kwa uzalishaji wake mkubwa wa koltani.

Eneo la Rubaya, mashariki ya Kongo ni kitovu muhimu cha madini ya coltanPicha: Baz Ratner/REUTERS

Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Angola mnamo Agosti, waasi wa M23 walianza tena mashambulizi tarehe 20 Oktoba, wakichukua mji wa Kalembe kwa muda mfupi huko Kivu Kaskazini kabla ya kufurushwa na wanamgambo wa Wazalendo na kundi la NDC-R, linaloongozwa na Guidon Shimiray Mwissa, mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita ambaye anashirikiana na jeshi la Congo.

Soma pia: M23 wauteka mji wa Kalembe mashariki ya Kongo

Mji wa Kalembe upo kwenye mhimili muhimu wa usafiri wa hifadhi ya madini miongoni mwa mambo mengine. Augustin Muesi, Profesa wa chuo kikuu ambaye anafundisha sayansi ya siasa mkoani Kivu Kaskazini, alisema eneo la Walikale ni tajiri sasa kwa madini, na kwamba ikiwa M23 wanataka kukalia eneo hilo kwa gharama yoyote, ni kwa lengo tu la kupata fursa ya kuchimba madini ili kuendelea kufadhili operesheni zake za kijeshi.

Makadirio ya UN yanaonyesha waasi wa M23 wanapata takriban dola 300,000 kwa mwezi kutokana na ushuru wa uzalishaji wa koltani katika wilaya za Masisi na Rutshuru. Mnamo Aprili 2024, M23 waliizingira Sake, ambayo kitovu cha usafiri karibu na Goma, na pia waliiteka Rubaya, mji muhimu kwa uchimbaji wa koltani, madini yenye umuhimu wa kimkakati hasa kwa mabadiliko ya nishati.

Waathiriwa wa mgogoro unaoendelea wamelazimika kuhamia kambi za wakimbizi wa ndani kama hii karibu na GomaPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Serikali ya Congo imeilaumu M23 kwa kusafirisha madini kutoka migodi ya Rubaya kwenda Rwanda kwa ajili ya uchakataji. Shirika moja la kiraia la eneo hilo limesema waasi wamegawa vifaa ili kuhimiza kuanza tena kwa shughuli za uchimbaji madini.

Ripoti ya hivi karibuni ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Congo inasema kuwa takriban wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wapo kwenye ardhi ya Congo kuwasaidia M23, ambao wana wapiganaji wapatao 3,000.

Wataalamu hao waliandika kuwa uingiliaji na operesheni za kijeshi za RDF katika wilaya za Rutshuru, Masisi, na Nyiragongo zilivuka msaada wa kawaida kwa M23, zikihusisha ushiriki wa moja kwa moja uliowezesha upanuzi wa haraka wa udhibiti wao hadi mwambao wa Ziwa Edward.

Kulingana na Mradi wa Takwimu za Maeneo na Matukio ya Migogoro ya Kijeshi, ACLED, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia migogoro duniani kote, vuguvugu la waasi la M23 limehusika katika matukio ya ghasia takriban 1,700 tangu kuanza tena shughuli zake mnamo Novemba 2021, na kusababisha vifo vya watu 1,746.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW