Waasi wa Mali 'waanzisha' utawala wa Kiislamu
3 Aprili 2012Mkaazi mmoja wa mji wa kihistoria wa Timbuktu, ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, kwamba wapiganaji hao wa Kiislamu wa kundi la Ansaruddin, wamevitaka vituo vya redio kuacha kupiga muziki na pia kutangaza wanawake waache kuvaa suruali za kubana na badala yake wavae kanzu.
Ansaruddin inachukuliwa kama vuguvugu la Kiislamu ambalo pamoja na Chama cha Ukombozi cha Azawad (MNLA), wamekuwa wakipigania uhuru wa eneo kaskazini mwa Mali.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), wakimbizi wa Mali wamekuwa wakivuuka mpaka na kuingia Burkina Faso na Mauritania kwa idadi ya watu 400 kwa siku, ndani ya kipindi cha wiki chache zilizopita.
Taarifa ya Shirika hilo iliyotolewa leo (Jumanne, 03.04.2012) imesema kwamba wengi wa wakimbizi hao wanatokea miji ya Timbuktu na Gao, ambayo yote iko mikononi mwa waasi, tangu wanajeshi wa serikali walipokimbia makambi yao. Taarifa hiyo inasema watu wanaokimbia wanahofia wizi wenye silaha na mapigano yanayoweza kuripuka, huku wengine wakikimbia njaa.
Njaa, ukosefu wa usalama na uhaba wa mafuta
Wakizungumza na DPA, wakaazi wa miji iliyo chini ya waasi, ya Timbuktu na Gao wamesema kwamba wana uhaba mkubwa wa chakula na mafuta ya petroli. Shirika la UNHCR limesema kwamba limepokea ripoti za watu wenye silaha kupora magari, mali na fedha.
Timbuktu ulikuwa mji wa mwisho kutwaliwa na waasi kati ya miji mitatu ya kaskazini mwa nchi hiyo, baada ya ule wa Gao na Kilad. Waasi wanapigania kulikomboa jimbo lao wanaloliita Azawad, ambalo linajumuisha eneo la mpaka wa Mali, Algeria na Niger, kilomita chache nje ya Timbuktu.
Mji wa kihistoria wa Timbuktu ni miongoni mwa turathi za kimataifa chini ya uangalizi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, ambao unatajwa kuwa na idadi kubwa ya maktaba zenye vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiarabu, vikizungumzia fani za falsafa za Kiafrika, haki za binaadamu na unajimu. Vitabu hivi havijawahi kuhifadhiwa katika mtindo wa sasa maandishi, na inahofiwa kwamba vinaweza kupotea baada ya serikali kupoteza udhibiti wa eneo hilo.
Wanajeshi wasaka suluhu
Katika hatua nyengine, tayari vikwazo vilivyotangazwa jana na Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, dhidi ya utawala mpya wa kijeshi wa Mali, vimeanza kuonesha makali yake kwa wananchi wa kawaida nchini humo, baada ya huduma muhimu za chakula na mafuta kuanza kuadimika.
Ujumbe maalum kutoka kiongozi wa mapinduzi ya Mali, Kapteni Amadou Sanogo, hivi leo ulikuwa mjini Abuja kwenye makao makuu ya ECOWAS kuwasilisha salamu za Kapteni Sanogo kwa viongozi wa Jumuiya hiyo.
Tayari Kapteni Sanogo alishaahidi kurejesha katiba ya nchi hiyo, katika jitihada zake za kutafuta uungwaji mkono na nchi jirani na jumuiya ya kimataifa, lakini ECOWAS imesema kiongozi huyo wa mapinduzi ameshindwa kutimiza ahadi zake.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman