Waasi wa Mali wajiondoa katika mchakato wa amani
27 Septemba 2013Taarifa ya pamoja kutoka kwa kundi la Tuareg na muungano wa waasi wa kiarabu imesema kufuatia matatizo chungu nzima katika utekelezaji wa makubaliano ya Ougadugou ambayo yanasababishwa na kushindwa kwa upande wa serikali kuheshimu mkataba huo,makundi hayo ya waasi yamejiondoa kutoka mchakato huo wa kutafuata amani nchini Mali.
Mkataba uliotiwa saini mwezi Juni mwaka huu katika nchi jirani ya Burkina Faso ulitoa fursa kwa jeshi la Mali kurejea katika mji mkuu wa jimbo la Kidal miezi 18 baada ya jeshi hilo kuutoroka mji huo kufuatia mashambulio makali kutoka kwa waasi.
Mapatano hayo ya Ougadougou yaliyomaliza mapigano ya miezi 18 nchini humo pia yalitoa fursa ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu mwezi Juni ambao Rais Keita alishinda.
Hata hivyo kumekuwa na dalili za mvutano kati ya pande hizo mbili.Mapema mwezi huu wanajeshi wa Mali walikabiliana na waasi wa kituareg karibu na mpaka wa Mauritania,makabiliano ya kwanza kati yao tangu kutiwa saini mkataba huo wa amani.
Kupatikana amani sasa kwatiliwa shaka
Chini ya mkataba huo,mazungumzo ya kutafuata amani yalipaswa kuanza mwishoni mwa mwezi Novemba kati ya serikali na waasi wa muungano NMLA ambao wanataka kujitenga na kuunda taifa jipya la Azawad, na makundi mengine mawili ya waasi ambayo pia yametangaza kujiondoa kutoka mkataba huo.
Muasisi wa NMLA Mossa Ag Acharatoumane ameishutumu serikali kwa kushindwa kutimiza upande wake wa makubaliano hayo baada ya jeshi kukubaliwa kuingia maeneo ya waasi.
Kufuatia mkutano mjini Ouagadougou,makundi manne ya waasi yamesema yanataka mkutano wa dharura wa pande zote husika ili kutathimini utekelezwaji wa makubaliano ya Ouagadagou.
Waasi hao wanaotaka kujitenga kwa eneo la kaskazini mwa Mali miongoni mwa masuala mengine wanaishutumu serikali kwa kukosa kuwaachilia wafungwa kama walivyokubaliana.
Serikali ya Mali haijatoa tamko lolote kuhusiana na uamuzi huo wa waasi ambao unahofiwa huenda ukaibua hali mpya ya mivutano.Wiki iliyopita waandmanaji katika mji wa Kidal waliwarushia mawe maafisa wa serikali mpya waliokuwa wameuzuru mji huo.
Waasi kutoka kabila la Tuareg wamekuwa wakitaka kujitenga kwa eneo hilo la kaskazini tangu Mali kujinyakulia uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960 na mwaka jana waliongoza uasi mkubwa uliosababisha machafuko mabaya kiasi cha Ufaransa kutuma jeshi lake kudhibiti hali ya mambo.
Mwandishi:Caro Robi/afp/ap/reuters
Mhariri: Daniel Gakuba