1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa mwisho waendelea kuondoka mji wa Homs

19 Machi 2017

Waasi hao waliokuwa wamebakia katika mji huo wa magharibi mwa Syria walianza kuondoka na familia zao mapema jana kuelekea katika mji mwingine wa Al - Wair uliopo kaskazini mwa Syria.

Infografik The refugee crisis in Syria after six years of war English

Mashirika ya habari na watu walioshuhudia zoezi hilo wamesema waasi na familia zao walisafirishwa kwa mabasi chini ya usimamizi na ulinzi wa Urusi. Kwa mujibu wa taarifa ya gavana wa mji huo,waasi kati ya 400 na 500 walianza kuondoka kutoka mji wa Homs. Zoezi hilo limetekelezwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya wawakilishi wa waasi na serikali ya Syria. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa watu kati ya alfu 10 hadi alfu 15 wanatarajiwa kuondoka mji huo mnamo muda wa wiki sita hadi miezi miwili.

Kitongoji cha Al -Wair kilichopo katika mji wa Homs ndicho kilichokuwa sehemu ya mwisho iliyokuwa inadhibitiwa na waasi.  Al-Wair ni sehemu yenye wakaazi alfu 75 na imekuwa inazingirwa na majeshi ya serikali tangu mwishoni mwa mwaka 2013. Kitongoji hicho kilizingatiwa kuwa makao makuu ya mapinduzi.  Gavana wa mji wa Homs Talal Barasi amesema wanajeshi wa Urusi waliliratibisha zoezi hilo na kwa mujibu wa makubaliano watahakikisha usalama katika njia itakayotumiwa na waasi. Wanajeshi wa Urusi hadi 100 watashiriki katika kuuhakikisha usalama wa watu hao wanaoondoka kutoka mji wa Homs. Mji huo ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini Syria ndio chimbuko la harakati za kuupinga utawala wa Assad. Mnamo mwezi wa Desemba mwaka 2015 waasi na serikali ya Syria walishakubaliana juu ya waasi hao kuondoka kwenye mji wa Homs ambao ulikuwa ngome kuu ya wapiganaji wanao endesha harakati za kupambana na utawala wa rais Bashar al Assad.

Waandamanaji wanaompinga rais AssadPicha: Reuters

Cheche za harakati.

Miaka sita iliyopita maalfu ya watu walikusanyika kwenye uwanja wa uhuru na kufanya maandamano ya kumtaka gavana wa jimbo la Homs aondolewe madarakani kutokana na kukabiliwa na madai ya kushiriki katika vitendo vya ufisadi. Majeshi ya serikali ya rais Bashar al Assad yalijibu kwa kufyatua risasi. Kwa mujibu wa habari waandamanaji zaidi ya 60 waliuwawa. Tangu wakati huo mji wa Homs ulikuwa unashambuliwa na majeshi ya Syria na sehemu kubwa ya mji huo imeteketezwa. Serikali ya Syria imesema utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika sehemu kadhaa zinazoshikiliwa na waasi ndio njia ya ufanisi ya kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyo ikumba Syria katika miaka sita iliyopita. Hata hivyo waasi wamesema wamelazimishwa kuikubali mikataba hiyo kutokana na kuzingirwa na kupigwa mabomu majeshi ya Syria. Mji wa Homs ulikuwa uwanja mkuu wa mapambano baada ya wakaazi wa mji huo kuitikia mwito juu ya kumpindua rais Assad uliotolewa na wanaharakati mnamo mwaka 2011.

Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: Reuters/Sana

Nani mshindi?

Rais Assad anaweza kusema kwa sasa yupo salama na kwamba yeye ndiye mshindi lakini vita vya nchini Syria havionyeshi ishara ya kumalizika hivi karibuni. Uamuzi wa rais wa Urusi Vladimir Putin wa kuongeza kwa kiwango kikubwa msaada wa kijeshi kwa rais Assad ulibadilisha urari wa nguvu za kijeshi nchini Syria kwa manufaa ya Assad. Kwa mujibu wa wachambuzi kiongozi huyo wa Syria bado hajashinda vita lakini wakati huohuo wachambuzi hao wanasema ni vigumu kwa waasi kushinda vita vya nchini Syria. Watu Zaidi ya 300,000 wameshauwawa tangu vita hivi vianze miaka sita iliyopita. Mamilioni wengine wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani.

Mwandishi: Zainab Aziz/ DPAE/RTRE

Mhariri: Isaac Gamba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW