1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Syria waidungua ndege ya jeshi la serikali

14 Agosti 2012

Waasi nchini Syria wamedai wameidungua ndege ya jeshi la serikali na kumteka rubani wake, huku mapigano yakiwa yanaendelea katika miji ya Damascus na Aleppo. Serikali imesema ndege hiyo ilipata matatizo ya kiufundi.

Ndege ya Syria iliyodunguliwa
Ndege ya Syria iliyodunguliwaPicha: Reuters

Kudunguliwa kwa ndege hiyo kumetangazwa na waasi kupitia picha zilizowekwa kwenye mtandao, ambao hata hivyo hazijathibitishwa na chombo kisichoegemea upande wowote. Picha hizo pia zinamuonyesha mtu ambaye waasi wanasema ni rubani wa ndege hiyo iliyodunguliwa, akiwa amezungukwa na wapiganaji wenye bunduki. Waasi wamesema watamtunza mtu huyo aliyejitambulisha kama Kapteni Abu Laith, kulingana na maadili ya kidini, na mikataba ya kimataifa.

Serikali imekanusha kudunguliwa kwa ndege hiyo, ikisema imeanguka baada ya kukumbwa na hitilafu za kiufundi ikiwa kwenye mazoezi.

Waasi washutumiwa kwa vitendo vya kinyama

Waasi wa Syria wameshutumiwa kuwafanyia unyama washirika wa serikaliPicha: Reuters

Picha nyingine lakini ambazo pia ziko kwenye mtandao, zimewaonyesha waasi hao wa Syria wakifanya vitendo vya kinyama mjini Aleppo, ambavyo vinaweza kuzifadhaisha nchi za magharibi zinazowaunga mkono wazi wazi. Katika mkanda mmoja, waasi hao wanaonekana wakizitupa kutoka kwenye paa la nyumba maiti wanazosema ni za wanamgambo wa Shabbiha, na pia maiti hizo zikizomewa na kukanyagwa kanyagwa na umati wa watu. Mkandsa mwingine unaonyesha kijana mmoja aliyekatwa koo akigaragara chini.

Waasi wanasema picha huenda picha hizo zimewekwa na serikali kwa malengo ya kuwapaka matope. Wanamgambo wa Shabbiha wanatoka hasa katika madhehebu ya Alawite kama rais Assad, na wameshutumiwa kuendesha mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa madhehebu ya Suni.

Ghasia hizi zilizodumu kwa muda wa miezi 17 zimesababisha wimbi kubwa la wakimbizi kuihama Syria na kutafuta hifadhi katika nchi jirani. Mojawapo ya kambi zilizowapokea ni Zaatari iliyoko nchini Jordan yenye mahema takribani 2000 karibu na mji wa mpakani wa Mafraq. Usiku wa kuamkia leo, wakimbizi waishio ndani ya kambi hiyo wamekabiliana na maafisa wa usalama wa Jordan, wakilalamikia hali katika kambi hiyo, ambayo wanasema haivumiliki.

Ripoti zimeeleza kuwa vurugu ziliripuka pale polisi wa Jordan walipompiga kijana mmoja wa Kisyria ambaye alijaribu kukimbia kutoka kambini humo. Mmoja wa wakimbizi waishio ndani ya kambi hiyo Abu Mohammed amesema hali kambini humo ni mbaya kuliko hata ile waliyoiacha nyumbani kwao.

''Tulikimbilia Jordan tukitaka kuisha maisha salama na ya heshima, si kuishi kama wanyama '' Alilalamika Mohammed.

Ujerumani yaahidi msaada

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel ameizuru Jordan kuangalia hali ya wakimbizi wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel ameitembelea kambi hiyo ya Zaatari, ili kupata picha halisi ya msaada unaohitajika. Akizungumza kambini humo, waziri Niebel amesema hana jibu la moja kwa moja juu ya hali inayoendela, lakini akaahidi msaada wa Ujerumani kuboresha maisha ya wakimbizi.

''Kwa sasa hakuna hatua ya dharura ninayoweza kuifikiria. Serikali ya Ujerumani inadhamiria kutoa msaada kuhakikisha kwamba mahitaji ya wakimbizi yanapatikana, na inataka kurejeshwa haraka kwa hali ya usalama ili wakimbizi hao waweze kurudi nyumbani.'' Alisema Niebel.

Baadaye ofisi ya Dirk Niebel mjini Berlin imetangaza msaada wa euro milioni 10, ambao utasaidia kuwapa maji safi wakimbizi wa Syria wapatao laki moja na nusu waliopo kaskazini mwa Jordan.

Huku hayo yakiarifiwa, mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Nchi za Kiislamu wenye wanachama 57, wamekubaliana kusimamisha uanachama wa Syria, kutokana na ukandamizaji unaoendelezwa na serikali ya Rais Bashar al Assad. Haya yameelezwa na katibu mkuu wa umoja huo, Ekmeleddin Ihsanoglu mjini Maka Saudi Arabia, wanakokutana mawaziri hao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/DPA

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW