1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Syria waondoka Quneitra

21 Julai 2018

Wapinzani 2,800 ambao pia ni waasi pamoja na familia zao wamekubali kuondoka Quneitra kufuatia makubaliano yaliyosimamiwa na Urusi

Syrien Deraa Al-Mal  Syrische Armee Eroberung
Picha: picture-alliance/Photoshot/X. Dezhi

Waasi 2,800 wa Syria pamoja na familia zao wameondoka katika mkoa wa kusini magharibi mwa Quneitra jana, kuelekea mkoa wa kaskazini magharibi wa Idlib, kufuatia makubaliano mapya yaliyosimamiwa na Urusi.

Hayo yamesemwa na kundi la uangalizi la haki za binadamu katika vita nchini Syria, lenye makao yake Uingereza likiongeza kuwa wanawake na watoto 1,700 ni miongoni mwa waliohamishwa.

Takriban mabasi 55 yaliondoka Quneitra yakiwa yamebeba kundi la kwanza la wapiganaji hao waliokataa kubaki katika eneo hilo.

Chini ya makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Urusi, waasi walikubali kuusalimisha kwa jeshi la Syria mkoa wa Quneitra ambao pia uko katika mpaka na milima ya Golan inayokaliwa na Israel. Pia walikubali kuzisalimisha silaha zao nzito.

Makubaliano kuhusu Quneitra ni ushindi mwingine muhimu kwa rais wa Syria Bashar al-Assad, ambaye katika miezi ya hivi karibuni, ameyakomboa maeneo mengi kusini mwa Syria.

Mwanajeshi wa Syria akionyesha ishara ya ushindi katika eneo la Al-Mal Hill kaskazini magharibi mwa DaraaPicha: imago/Xinhua/Xu Dezhi

Kwa mujibu wa kundi hilo la uangalizi, makubaliano hayo hayakujumuisha kundi la wapiganaji wa Hayat Tahrir al-Sham.

Huku hayo yakijiri, kundi la uangalizi la haki za binadamu limesema ndege za kivita za Urusi zimeendelea kufanya mashambulizi makali katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Khaled bin Walid ambaye ni mshirika wa kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu-IS magharibi mwa Deraa

Ndege hizo zililenga vijiji vya Heet na Taseel na kuwaua watu 26 wakiwemo watoto 11. Mapema siku ya Ijumaa, makubaliano ya kuwaondoa watu katika miji miwili inayoiunga mkono serikali lakini iliyozingirwa na waasi yalikamilishwa.

Rami Abdel Rahman ambaye ni mkuu wa shirika la uangalizi wa haki za buinadamu la Syria ameliambia shirika la habari la DPA kuwa, makubaliano ya al-Foua na Kfarya yalitimizwa na mabasi yote yaliingia katika maeneo ya utawala, huku mamia ya wafungwa wa upinzani walioachiliwa huru wakiingia katika ngome za waasi.

Watu waonekana wakiondolewa kutoka vijiji vya al-Foua na Kefraya SyriaPicha: Reuters/K. Ashawi

Ameongeza kuwa waliohamishwa wameelekea katika makazi ya muda mfupi ya Jibreen karibu na mji wa Aleppo kaskazini mwa Syria.

Mnamo Alhamisi, tofauti iliibuka kuhusu wafungwa wa upinzani walioshikilia mabasi 23 yaliyowabeba watu kutoka vijiji viwili vinavyounga mkono serikali karibu na kivukio cha Ays katika vijiji vya Aleppo.

Tofauti hiyo ilitokea pale waasi walilalamika kuwa baadhi ya hao walioachiliwa walikuwa wafungwa waliokamatwa hivi karibuni na utawala ulioko madarakani na si wanachama wa kundi la Al-Qaeda linalohusishwa na Hayat Tahrir al_Sham lilivizingira vijiji viwli vinavyopendelea serikali.

Kwa mujibu wa kundi la uangalizi la haki za binadamu, takriban mabasi 120 yamewabeba watu 6,900 kutoka vijiji vinavyounga mkono serikali

Mwandishi: John Juma/DPEA
Mhariri: Bruce Amani

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW