1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Tigray wakubali kusitisha mapigano kwa masharti

5 Julai 2021

Viongozi wa waasi katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia wamekubali kusitisha mapigano, lakini wameweka masharti magumu ili makubaliano yaweze kufikiwa rasmi kabla hawajashiriki mazungumzo yoyote na serikali kuu.

Äthiopien | Jubel beim Einmarsch der TDF in Mekelle
Picha: DW

Miongoni mwa masharti yaliyowekwa na viongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF ni pamoja na kuondoka kwa vikosi vya Eritrea na wapiganaji kutoka jimbo jirani la Amhara, ambao wamekuwa wakiliunga mkono jeshi la Ethiopia katika mzozo uliodumu kwa miezi minane. Viongozi hao pia wametoa wito wa kurejeshwa kwa serikali yao ya Tigray iliyovunjwa, ambayo serikali ya shirikisho ya Ethiopia inaichukulia kama serikali ya waasi.

Tigray limekuwa eneo la mapigano tangu Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipolipeleka jeshi lake mwishoni mwa mwezi Novemba, kuiondoa madarakani serikali ya waasi wa TPLF. Abiy amekuwa akikishutumu chama hicho kwa kupanga mashambulizi katika kambi za jeshi la Ethiopia.

Usaidizi wa vikosi vya Amhara na Eritrea 

Jeshi la Ethiopia limekuwa likiungwa mkono na majeshi kutoka jimbo jirani la Ahmara na jeshi la Eritrea, nchi inayopakana na Tigray. Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kiutu, OCHA hivi karibuni ilisema kwa kiasi kikubwa vikosi vya Eritrea vimeondoka Tigray na kurejea kwenye eneo la mpaka.

Siku ya Jumatatu, waasi wa TPLF waliudhibiti tena mji mkuu wa Tigray, Mekele, ambao umekuwa chini ya jeshi la Ethiopia tangu Novemba 28, mwaka uliopita. Serikali ya Ethiopia mjini Addis Ababa mara moja ilitangaza kusitisha mapigano ya upande mmoja, lakini waasi wa TPLF waliikosoa hatua hiyo wakisema ni ya mzaha na waliapa kuendeleza mapigano.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: John Thys/AP/picture alliance

TPLF imesema wanataka kuhakikishiwa kwamba usalama wa watu wao hautavurugwa kwa uvamizi wa mara ya pili, na hilo likifanyika watakubali kusitisha mapigano. Taarifa ya waasi iliyotolewa siku ya Jumapili, imeeleza kuwa kabla ya makubaliano kuwa rasmi, changamoto hizo inabidi zitafutiwe ufumbuzi. TPLF inasema serikali yake ilichaguliwa kidemokrasia na watu wa Tigray na inataka kuanza kutekeleza shughuli zake za kikatiba.

Makubaliano yaheshimiwe

Umoja wa Mataifa na serikali za nchi kadhaa zimetoa wito wa kuheshimiwa kwa makubalino ya kusitisha mapigano na hasa kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia raia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu mzozo wa Tigray, akisema ni muhimu kusitisha mapigano na kuruhusu njia ya kufanyika mazungumzo.

''Uwepo wa majeshi ya kigeni ni jambo linalochochea mapigano. Na wakati huo huo, upatikani kamili wa msaada wa kibinaadamu bila kuwepo vizuizi lazima uwe wa uhakika kwenye eneo lote. Na uharibifu wa miundombinu ya raia haukubaliki kabisa,'' alisisitiza Guterres.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 400,000 wanakabiliwa na njaa jimboni Tigray na watu milioni 1.8 wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa.

Katika mkutano wa faragha na wanadiplomasia uliofanyika siku ya Ijumaa, viongozi wa Ethiopia walisema serikali iko tayari kufanya mazungumzo ya kuutatua mzozo wa Tigray, huku wakirudia kusema kwamba haitawashughulikia viongozi wa TPLF.

(AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW