Waasi wa Yemen waizingira nyumba ya Waziri Mkuu
20 Januari 2015Mapigano hayo yalizuka jana jioni kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa, baada ya walinzi wa rais kuwafyatulia risasi waasi wa Houthi waliokuwa katika doria, ambao waliikaribia Ikulu iliyopo kusini mwa mji huo.
Afisa wa waasi wa Kishia Houthi, Ali al-Quhum amesema wapiganaji wa kundi hilo, ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakiidhibiti Sanaa tangu mwezi Septemba, walikuwa wakijilinda. Wakaazi wa Sanaa wamesema kikosi cha ulinzi wa rais, kimeweka vifaru vya kijeshi kuizunguka Ikulu.
Hata hivyo, Rais wa Yemen, Abd Rabu Mansour Hadi, anayeungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mataifa ya Ghuba, hakuwepo Ikulu wakati mapigano hayo yanatokea.
Waziri wa Habari wa Yemen, Nadia Sakaff amesema kupitia mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Twitter, kwamba Rais Hadi, leo ameitisha mkutano wa makundi ya kisiasa, wakiwemo wapiganaji wa Houthi, kwa lengo la kuweka mikakati ya kumaliza mzozo uliopo.
Yemen yasema hilo ni jaribio la mapinduzi
Aidha, waziri huyo amesema hatua hiyo ya waasi ni jaribio la kutaka kuipindua serikali. Amebainisha kuwa watu wanane wameuawa na wengine 32 wamejeruhiwa katika mapigano hayo. Shirika la habari la Yemen, Saba, awali lilimkariri Waziri wa Afya, Yassin Abdullah akisema kuwa watu 55 wanatibiwa majeraha.
Msafara ulokuwa ukiwarudisha Waziri Mkuu wa Yemen, Khalid Bahah na ule wa mshauri wa zamani wa rais kutoka kundi la Houthi, Salih al-Samad kutoka kwenye mazungumzo ya dharura ya kusitisha mapigano, ulishambuliwa.
Tangazo la kusitisha mapigano lilitolewa baada ya watu walioshuhudia kusema kuwa waasi wanaidhibiti milima muhimu ambayo ni rahisi kuiona Ikulu na kambi hiyo ya kijeshi iliyoko kusini mwa milima hiyo.
Mataifa ya Magharibi ambayo ni washirika wa Yemen pamoja na washirika wa kimataifa, ikiwemo Marekani na Saudi Arabia, zimetaka hatua madhubuti zichukuliwe ili kutekeleza na kuimarisha makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, wakielezea namna wanavyomuunga mkono Rais Hadi.
Mvutano umekuwa ukiongezeka Sanaa tangu waasi wa Houthi walipomteka nyara mkuu wa majeshi katika serikali ya Rais Hadi, Ahmed Awad bin Mubarak, kwa lengo la kumzuia kiongozi huyo kukiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuundwa serikali mpya na uteuzi wa waasi wa Houthi kama washauri wa rais.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,APE, AFPE
Mhariri:Iddi Ssessanga