1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi waangusha ndege ya serikali, Syria

14 Februari 2020

Waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki wameidungua helikopta ya serikali mashariki ya Aleppo, kaskazinimagharibi mwa Idlib nchini Syria ambako kumeibuka mashambulizi katika wiki za karibuni.

Syrien Idlib Helikopter Abschuss
Picha: DHA

Tayari zaidi ya watu 800,000 wameyakimbia makazi yao katika eneo la kaskazinimagharibi mwa Syria tangu katikati ya mwezi Disemba kutokana na mazingira mabaya yaliyosababishwa na kampeni ya kijeshi ya serikali katika eneo la mwisho linalodhibitiwa na wassi nchini humo hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa.

Chanzo cha jeshi la waasi pamoja na mashuhuda wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba ndege za Urusi zilizokuwa zinayalenga maeneo yaliyoko magharibi mwa Aleppo mapema hii leo, zililazimika kurudi katikati ya mji baada ya kuangushwa kwa helikopta hiyo ya serikali.

Jeshi la Uturuki lilipeleka silaha za nyongeza na wanajeshi katika mkoa wa Idlib ili kuüambana na wanajeshi wa Syria wanaoungwa mkono na Urusi katika harakati za kulirejesha eneo hilo mikononi mwa serikali.

Watoto ni miongoni mwa wakimbizi wa ndani wanaoteseka zaidi nchini Syria Picha: Getty Images/AFP/A. Watad

Misaada ya kiutu imeanza tena kuingia Idlib baada ya kusubiri kwa muda mrefu kufuatia kuibuka upya kwa mapigano. Msemaji wa shirika la chakula ulimwenguni, WFP Elisabeth Byrs amesema "Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa msaada wa dharura wa chakula kwa watu wenye mahitaji makubwa ya chakula kaskazinimagharibi mwa Syrialicha ya kusambaa kwa machafuko."

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali mbaya ya raia wa Idlib.

Amesema, malori yenye vyakula yamerejesha huduma zake za kugawa chakula baada ya kusubiri kwa masaa 24 na kuongeza kuwa hali hiyo inadhihirisha wazi ugumu wanaokutana nao katika kuwasaidia watu ambao hawana makazi.

Wakati haya yanatokea mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na Uturuki wanataraji kukutana kwa mazungumzo mjini Munich, hii ikiwa ni kulingana na Urusi. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu watakutana pembezoni mwa mkutano wa usalama mjini humo taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema.

Shirika la mahusiano ya kiutu la Umoja wa Mataifa, OCHA limesema zaidi ya watu 800,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini Syria kutokana na hali mbaya kufuatia mashambulizi hayo.  Ripoti ya Umoja wa Umoja wa Mataifa iliyochapishwa jana jioni imesema wanawake na watoto ambao ni asilimia 81 ya idadi hiyo mpya ya wakimbizi wa ndani ndio wanaoteseka zaidi. 

Aidha shirika hilo limeonya kuhusu matatizo yanayowakabili wakimbizi hao wa ndani yanatokana na baridi kali. Tayari watu watano wamekufa kutokana na baridi kali, hii ikiwa ni kulingana na OCHA. Limetoa mwito wa dharura ya upatikanaji wa makaazi, katika wakati ambao mamilioni wamelazimishwa kujirundika kwenye maeneo madogo na ambayo hayana vifaa vya kujikinga na baridi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW