1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wakabiliwa Mali

MjahidA1 Aprili 2013

Vikosi vya Mali, vikisadiwa na jeshi la Ufaransa, vimefanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa itikadi kali za kidini katika eneo la Timbuktu, baada ya kupambana nao hapo jana na kusababisha mauaji ya watu 7.

Waasi wa Mali
Waasi wa MaliPicha: picture alliance / AP Photo

Kufikia jana jioni utulivu ulikuwa unashuhudiwa katika eneo la Timbuktu baada ya wapiganaji hao wa Kiislamu kuanza kukabiliana na jeshi la Ufaransa pamoja na lile la Mali, muda mfupi baada ya mripuaji wa kujitoa muhanga kujiripua siku ya Jumamosi katika kizuizi cha polisi.

Katika mapambanao hayo, watu saba waliuwawa wakiwemo waasi wanne, mwanajeshi mmoja na raia wawili.

"Kwa sasa kumetulia mjini Timbuktu na kila kitu kiko shwari kabisa, sasa tumelidhibiti eneo hili," Alisema afisa mmoja kutoka Mali alipokuwa anazungumza na shirika la habari la AFP.

Wanajeshi wa MaliPicha: Getty Images

Kulingana na raia mmoja anayeishi katika mji huo, hawasikii tena milio ya risasi lakini kila mtu amejifungia nyumbani kwake, baada ya mapigano kuanza siku ya Jumamosi jioni.

Jeshi la Mali limesema limetuma kikosi katika eneo hilo kuangalia iwapo kuna wapiganaji wowote wa Kiislamu waliobakia.

Mapambano ya waasi

Awali wapiganaji hao waliingia katika mji huo ambao ulikombolewa na jeshi la Mali kwa usaidizi wa jeshi la Ufaransa miezi michache iliyopita na kuanza kufyatua risasi wakilenga kambi ya jeshi ya Mali na hoteli moja ambayo inatumika kama makaazi ya muda ya gavana.

Mmoja wa waasi, MaliPicha: Reuters

Habari iliyotolewa na afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe imesema raia mmoja wa Nigeria aliyekuwa ameshikwa mateka pia aliuwawa katika mapambano hayo.

Kwa sasa Gavana wa eneo hilo pamoja na waandishi habari wawili wa kimataifa wamehamishwa kutoka katika hoteli iliyokuwa imelengwa na wapiganaji hao.

Kamisheni ya amani yaundwa

Hapo jana kiongozi wa mpito wa Mali Dioncounda Traore alimteua Mohamed Salia Sokona ambaye ni waziri wa zamani wa Mali na balozi mstaafu kuongoza kamisheni mpya iliyopewa majukumu ya kuhimiza amani katika eneo hilo. Kamisheni hiyo itakuwa na wajumbe 30.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius, anayetarajiwa kuwa ziarani nchini Mali hapo tarehe 5 Aprili amepongeza uteuzi wa kamisheni hiyo na kusema kuwa ni hatua muhimu katika kuleta amani na kuwa na makubaliano ya kisiasa.

Kiongozi wa mpito Mali Dioncounda TraorePicha: picture-alliance/dpa

Mali imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji hao tangu Ufaransa ilipoiingilia kijeshi nchini humo kuisaidia kutodhibitiwa na waasi waliokuwa wanaelekea kulichukuwa eneo zima la kaskazini mwa nchi hiyo. Waasi walipata nafasi hiyo baada ya mapinduzi yaliyofanywa na anajeshi walioasi mwezi Machi mwaka 2012.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW