Waasi wataka kusitishwa kwa mapigano nchini Libya
1 Aprili 2011Televisheni ya Shirika la Habari la Uingereza, BBC imemnukuu daktari mmoja nchini Libya akisema watu 7, miongoni mwao wakiwemo watoto wameuwawa huku wengine 25 wakijeruhiwa vibaya karibu na mji wenye hazina ya mafuta wa Brega.
Daktari huyo amesema alitakiwa aende katika kijiji kimoja kilichopo umbali wa kilometa 15 kutoka Brega, muda mfupi baada ya ndege za majeshi ya muungano kushambulia vikosi vinavyomuunga mkono Kanali Ghadhafi.
BBC imesema mabaki ya makombora yameonekana katika nyumba mbili tofauti ambapo, wameuwawa wasichana wawili na mvulana wa umri kati ya miaka 12 na 20.
Jumuiya ya Kujihami ya NATO imechukua jukumu kamili la kuendesha operesheni ya mashambulizi ya anga kwa lengo la kuvuruga mfumo wa kijeshi wa Libya ikiwa ni matakwa ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ripoti ya tukio hilo la mauji inatolewa wakati Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen akiwa tayari katangaza umakini wa utekelezaji wa opereshini hiyo."Nato itashiriki kikamilifu kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,nalo ni tutakuwa huko kuwalinda Walibya, wala si kudhuru."alisema Rasmussen.
Huko Benghazi,Kiongozi wa Baraza la Mpito la Waasi,Mustafa Abdul Jalil amekutana na Ujumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa unaongozwa na Abdul Ilah Khatib.
Akizungumza muda mfupi baada ya kukutana na ujumbe huo,Jalil amesema wapo tayari kusitisha mapigano kwa masharti kwamba mamlaka ya Ghadhafi itoe uhuru wa kujieleza kwa raia wa nchi hiyo pamoja na kuviondoa vikosi vyake katika makazi ya watu.
Naye Kiongozi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa,Khatib amesema lengo kubwa la kuwasili nchini Libya ni kufanikishwa usitishwaji wa mapigano nchini humo.
Taarifa nyingine zinaeleza vikosi vinavyomuunga mkono Kanali Gaddafi vinafanya mashambulizi katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Misrata.
Akizungumza na Shirika la Habari la Uingereza, Reuters kwa njia ya simu, msemaji wa waasi mjini humo anadai vikosi hivyo vikiwa na silaha nzito vikiwemo vifaru vinavamia makazi ya watu na maduka na kuharibu kila wanachokiona katikati ya mji huo.
Wakati hali bado ni tete, taarifa nyingine zinaeleza maafisa upande wa waasi wamesema wamekubaliana na taifa la Kiarabu la Qatar kwamba litawapa fedha za kununulia silaha na bidhaa nyingine ili liweze kuuza mafuta.
Kauli hiyo inatolewa muda mfupi baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates kusema."Hakutakuwa na uungwaji mkono wa mapigano ya ardhini nchini Libya"
Al Tarhouni, ambaye ni mkuu wa biashara katika Baraza la waasi amesema Qatar imekubali kuuza mafuta yaliyo katika himaya yao kwa makubaliano hayo huko eneo la kusini mwa Libya.
Mwandishi-Sudi Mnette/RTRE/AFPE
Mhariri: Josephat Charo