Waasi watumia binadamu kama ngao
3 Novemba 2015Wakati huo huo Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeyashutumu makundi ya waasi nchini Syria kwa uhalifu wa kivita.
Ndege za kivita za Urusi zimeshambulia maeneo ya kundi la Dola la Kiislamu katika eneo la Tadmur katika jimbo la Homs, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema , ikitumia jina la Kiarabu kuutaja mji wa Palmyra.
Kutokana na mashambulizi hayo , handaki la kundi hilo pamoja na silaha za kutungulia ndege zimeharibiwa , taarifa hiyo imesema. Rami Abdel Rahman , mkuu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza , pia amesema kwamba ndege za kivita za Urusi zimeshambulia mji wa kale wa Palmyra jana.
Mji wa Kihistoria wa Palmyra
Wizara ya ulinzi ya Urusi hapo kabla ilisema kwamba ndege zake zilishambulia karibu na mji huo lakini imesisitiza kwamba imeepuka kuushambulia mji huo wa kihistoria.
Mshauri wa makamu mwenyekiti wa baraza la taifa nchini Urusi Andrei Baklanov amesisitiza kwamba mashambulizi yao yanaathiri shughuli za waasi.
"Licha ya kuwa mashambulizi ya anga yameleta mabadiliko kidogo katika uwanja wa vita na kukamata asilimia sita tu ya maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na magaidi , kwa kiasi kikubwa yanaathiri makundi ya kigaidi."
Shirika la Human Rights Watch limewashutumu waasi nje ya mji mkuu Damascus kwa uhalifu wa kivita baada ya kuwaweka mateka wao ikiwa ni pamoja na raia katika masanduku ya waya na kuwatumia kama ngao ya binadamu dhidi ya mashambulizi ya majeshi ya serikali.
Ngao ya binadamu
Vidio zilizowekwa katika mtandao mwishoni mwa juma zinaonesha mateka hao, miongoni mwao wanajeshi na raia , wakiwa katika masanduku ya waya wakisafirishwa katika maeneo mbali mbali katika jimbo la mashariki la Ghouta nje ya mji wa Damascus.
Shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria limesema kundi lenye nguvu la Jaish al-Islam limewaweka watu hao katika masanduku hayo katika maeneo ya wazi kuzuwia majeshi ya serikali kushambulia kwa mabomu maeneo hayo.
Kundi Human Rights Watch la kutetea haki za binadamu limesema , hatua hiyo ni sawa na na kuwateka watu na kukasirishwa kwa kuwa inawavunjia hadhi yao ya kiutu, na kwamba hali hiyo ni sawa na uhalifu wa kivita.
Wakati huo huo jopo la Umoja wa Mataifa litaanza hivi karibuni kazi ya kuwatafuta wale wanaohusika na mashambulizi ya gesi ya sumu nchini Syria, lakini mkuu wa uchunguzi amesema itakuwa vigumu kuwapata wote waliohusika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman