1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binaadamu wafidiwa Kenya

Shisia Wasilwa
15 Juni 2026

Waathiriwa wa matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu waliopata madhara wakati wa maandamano nchini Kenya wataanza kupokea fidia ya serikali kuanzia wiki ijayo.

Kenia Nanyuki 2026 | Proteste gegen US-gestützte Ebola-Quarantäneeinrichtung
Waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binaadamu kupata fidia, Kenya Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Hatua hiyo inajiri majuma machache baada ya waathiriwa wa maandamano kutishia kuingia mitaani kuandamana kwa kile walichokitaja ni kuchelewa kwa serikali kuwafidia.

Wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR), Claris Ogangah, alisema mchakato huo unalenga kurejesha imani ya wananchi na kujenga upya mshikamano wa kitaifa.

Watakaonufaika na fidia hiyo ni Pamoja na waathiriwa wa maandamano ya vurugu yaliyojitokeza katika kipindi cha baada ya uchaguzi wa 2017 na 2022, pamoja na wale waliodhurika katika maandamano ya Mswada wa Fedha wa 2023, 2024 na maandamano ya Saba Saba ya 2025.

Waandamanaji Kenya, walipokuwa wanapinga ujenzi wa kituo cha Karantini cha kuhifadhi wagonjwa wa  Ebola wa raia wa Marekani.Picha: Luis Tato/AFP

Mama Grace Wanjiru alimpoteza mwanaye kwenye maandamano ya hivi karibuni katika eneo la Laikipia, waandamanaji walipopinga ujenzi wa kituo cha Karantini cha kuhifadhi wagonjwa wa  Ebola raia wa Marekani.

"Naomba haki kwa Charles, yeye hakuwa anaandamana lakini alikuwa anaeelekea kazini alipouawa kwenye maandamano.”

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa fidia, Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu imepokea zaidi ya visa  2,800. Tume hiyo tayari imehakiki na kuvijumuisha visa hivyo katika makundi sita ya ukiukaji wa haki.

Rais Ruto asema ni wakati wa uwajibikaji

Makundi hayo ya ukiukaji yanajumuisha vifo, majeraha, kukamatwa, ukatili wa kingono na uharibifu wa mali. Rais William Ruto amesema serikali yake imetenga shilingi bilioni mbili za Kenya kuwafidia waathiriwa wa maandamano hayo.

" Tumepuuza suala hili kwa muda mrefu, ni wakati kama taifa na mimi kama kiongozi wa taifa, kuwajibika na kufanya jambo kulihusu.”

Rais wa Kenya William Ruto Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Hata hivyo, ripoti hiyo imeelezea kuwa si kila kisa kilichoripotiwa kilikidhi vigezo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa ajili ya fidia, kwani baadhi vilihusisha matendo ya jinai ya kawaida. Visa hivyo vitashughulikiwa kupitia mfumo wa sheria za jinai.

Mashirika ya haki za binadamu kwa muda mrefu yamekuwa yakieleza kuwa waathiriwa wengi na familia zao wameachwa bila fidia ya kutosha au kutambuliwa kwa madhara waliopitia. Hussen Khalid ni Afisa Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa.

"Ikiwa unamlipa mtu fidia, inaonyesha kuwa umekubali umemkosea, basi tuone ule msamaha ukitoka, pili waliotekeleza makosa wachukuliwe hatua na kuwe na mabadiliko kuzuia matukio kutokea tena.”

Ripoti hii inakuja katika mazingira ya kuongezeka kwa wito wa uwajibikaji kufuatia matukio ya ukatili wa polisi, utekaji nyara na watu kupotezwa kwa lazima, mauaji yasiyo halali, mateso na ukiukaji mwingine unaohusishwa na machafuko ya kisiasa na maandamano ya umma. 

Kwa miaka mingi, tume mbalimbali za uchunguzi, mahakama na mashirika ya haki za binadamu zimechapisha matukio ya mauaji ya kiholela, ukandamizaji wa kisiasa, mateso, watu kutoweshwa kwa lazima, na ukiukaji mwingine. Hii itakuwa mara ya kwanza katika historia kwa waathiriwa kufidiwa iwapo hilo litatekelezwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW