1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabrazil kumchagua rais na wabunge leo

5 Oktoba 2014

Raia wa Brazil wanakwenda kwenye vituo vya kupigia kura leo, kumchagua rais na wabunge, huku kura za maoni zikiashiria kwamba rais wa sasa Bi Dilma Roussef kupata ushindi licha ya changamoto nyingi zinazomkabili.

Wagombea wa urais Brazil wakishiriki mdahalo mapema mwezi huu
Wagombea wa urais Brazil wakishiriki mdahalo mapema mwezi huuPicha: picture-alliance/dpa/Antonio Lacerda

Bi Roussef anayo sifa ya kuwa mtu wa mapambano. Aliwahi kufungwa jela kwa sababu za kisiasa, ameweza kuishi na kitisho cha ugonjwa wa saratani, alinusurika maandamano makubwa dhidi ya serikali yake mwaka 2013, na sasa anaonekana kuhimili vishindo vya kushtukiza vya mpinzani wake Bi Marina Silva, ambaye aliingia katika kinyang'anyiro cha urais baada ya kifo cha kiongozi wa chama chake ambaye alifariki katika ajali ya ndege.

Wachambuzi wanasema ni vigumu kutabiri nani atakuwa mshindi katika uchaguzi huu. Wiki chache zilizopita nyota ya Dilma Roussef ilikuwa imefifia, huku kura za maoni zikitabiri kuwa atalazimika kuingia duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya Marina Silva, ambaye alipewa nafasi kubwa ya kumbwaga Roussef.

Nyota ya Roussef yang'ara

Lakini, Bi Roussef amebadilisha mkondo wa mambo kwa kufanya kampeni kubwa, akitilia mashaka uwezo wa mshindani wake huyo. Mashaka hayo yameuporomosha umaarufu wa Marina katika muda mfupi.

Dilma Roussef, rais wa sasa ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda tenaPicha: Reuters

Matokeo ya kura za maoni yaliyochapishwa jana Jumamosi na wakala mbili muhimu za Datafolha na Ibope, zimeonyesha Bi Dilma Roussef akiwaongoza wapinzani wake kwa asilimia 20, ingawa zilionyesha pia kuwa asingeweza kupata kura za kutosha kumwezesha kupata ushindi wa moja kwa moja, kuepuka duru ya pili iliyopangwa kufanyika tarehe 26 Oktoba.

Mgombea wa tatu katika kinyang'anyiro hiki cha urais wa Brazil ni Aecio Neves kutoka chama cha Social Democracy, mtaalamu wa uchumi na mjukuu wa mwanasiasa maarufu Tancredo Neves. Aliwahi kuwa Gavana wa jimbo la Minas Gerais ambalo ni la pili kuwa na idadi kubwa ya wakazi nchini Brazil.

Matokeo ya kura za maoni Jumamosi yalimuonyesha yeye na Marina Silva wakikaribiana kwa kiwango cha kura wanazoweza kuambulia, cha kati ya asilimia 24 na asilimia 26, na kubashiri kuwa yeyote atakayekuja ya mwingine, ataangushwa na Roussef katika duru ya pili.

Marina Silva, mgombea anayempa changamoto RoussefPicha: Reuters/Nacho Doce

Teknolojia yatumiwa kupigia kura

Upigaji kura unafanyika katika mfumo wa elektroniki, na matokeo yatajulikana saa chache baada kufungwa kwa vituo saa kumi na moja jioni. Kupiga kura ni wajibu wa kisheria kwa wabrazil wenye umri wa kati ya miaka 18 na 70. Wa walio chini ya umri wa miaka 16, na waliopita umri wa miaka 70, kupiga kura ni hiari.

Mgombea wa tatu kanyang'anyiro, Aecio NevesPicha: Reuters/Nacho Doce

Chama cha wafanyakazi cha Dilma Roussef kimekuwa madarakani tangu mwaka 2002. Kwanza alichaguliwa mtangulizi wake Luiz Inacio Lula da Silva.

Kwenye siku ya mwisho ya kampeni jana Jumamosi, Dilma Rouissef alijikita katika jimbo la mpinzani wake wa karibu Marina Silva, ambako amejiimarisha kama mgombea anayependwa zaidi. Wakati huo huo Silva alielekeza juhudi zake katika mji wa Sao Paolo ambako anaonekana kuburura mkia. Neves kwa upande wake alifuata nyao za Roussef katika jimbo la Minas Gerais akijaribu kuvutia kura zote ambazo zinaweza kumsaidia kushiriki katika duru ya pili.

Wapigaji kura wanasema ni vigumu kuamua nani wa kumpa kura, lakini bila shaka kauli ya mwisho ni ya wapiga kura hao wapatao milino 143 katika nchi hiyo kubwa zaidi kieneo na kiuchumi katika bara la Amerika Kusini.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/afpe

Mhariri: Bruce Amani

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi