1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge Kongo wapiga kura kumuondoa waziri mkuu Ilunga

Admin.WagnerD28 Januari 2021

Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Jumatano limepiga kura kumuondoa madarakani waziri mkuu Sylvestre Ilunga Ilukamba, hatua inayoivunja serikali na kumpa rais Felix Tshisekedi fursa ya kuwateua watu wake.

Sylvestre Ilunga Ilunkamba des. Premierminister DR Kongo
Picha: Presidence RDC

Mwezi uliopita rais Tshisekedi alichukuwa hatua ya kuvunja muungano ulioundwa na mtangulizi wake, Joseph Kabila, ambao ulibana kimamlaka tangu alipoingia madarakani Januari 2019. Mvutano huo ndiyo uliochochea kura iliyopigwa na wabunge ya kutokuwa na imani na waziri mkuu, na kumaliza udhibiti wa Kabila serikaini. Kura hiyo iliungwa mkono na wabunge 367 kati ya 377 waliokuwepo bungeni.

"Serikali ya Waziri Mkuu Ilunga Ilunkamba sasa imejiuzulu. Waziri Mkuu anatakiwa kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa rais na serikali yake katika muda wa saa 24," alitangaza spika Mboso Nkodia Puanga baada ya mchakato wa kura kukamilika bungeni.

Washirika wa Kabila, akiwemo Ilunga, walisusia kura hiyo, wakisema spika wa mpito hakuwa na mamlaka ya kikatiba kusimamia muswada wa kutokuwa na imani na waziri mkuu.

Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilunkamba akiwa na Rais Felix TshisekediPicha: Presidence RDC

Kushindwa kujiuzulu kutazua ghasia

Kushindwa kujiuzulu kwa waziri mkuu hadi Alhamisi, kunaweza kukaitumbukiza nchi kwenye mzozo wa kisiasa kama ilivyokuwa mwaka 1960-1965 baina ya rais Joseph Kasavubu na waziri mkuu Patrice Emery Lumumba ambapo ilibidi nguvu zitumike.

Katika barua aliyomtumia rais siku ya Jumatano, Ilunga alisema hatojiuzulu kabla ya kuchaguliwa kwa spika wa kudumu, nafasi ambayo uchaguzi wake umepangwa kufanyika wiki ijayo. Lakini wanachotaka Wakongomani ni mabadiliko katika maisha yao ya kila siku.

"Nangoja nione serikali itakayoleta mabadiliko na kuruhusu watu kupumua. Sisi Wakongomani tunachokitafuta ni mabadiliko tu hapa nchini. Tangu Tshisekedi na serikali kuteuliwa hatujaona hatua zozote za kuboresha maisha. Tunataka sasa serikali itakayojibu mahitaji ya watu," amesema mkazi mmoja wa mji mkuu wa Kinshasa.

Muungano mpya wa kisiasa wa Rais Tshisekedi, maarufu kama Sacred Union, utampa rais wingi mkubwa katika bunge ingawa Kabila atabakisha ushawishi juu ya idara za usalama nchini humo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW