Wabunge Marekani kumchagua spika mpya
3 Januari 2023Kiongozi wa chama cha Republican katika Baraza la wawakilishi nchini Marekani Kevin McCarthy anapambana kuukabili upinzani wa msimamo mkali wa kihafidhina na kupata kura za kutosha za kumpa nafasi ya uspika.
Baada ya matokeo mabovu kuliko ilivyotarajiwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula, Warepublican wa McCarthy wamejikuta katika ugomvi wa umma kuhusu nani anapaswa kukiongoza chama chao wakati kitachukua udhibiti wa Bunge.
Soma pia: Marekani: Wademocrat kuendelea kudhibiti baraza la seneti
Kundi la wahafidhina wenye msimamo mkali linapinga ugombea wa McCarthy, kwa kuhofia kuwa anajihusisha sana na vita vya kitamaduni na ushindani wa vyama ambao umetawala bungeni na hata Zaidi tangu miaka ya Donald Trump akiwa Ikuluni.
Wanamkosoa Mrepublican huyo wa Carlifornia kwa kutochukua msimamo dhabiti dhidi ya Wademocrat, ambao chini ya Spika Nancy Pelosi walikuwa katika udhibiti, kuhusu vipaumbele vikiwemo ufadhili wa serikali, ulinzi na usalama wa mipakani.
Mwakilishi Bob Good ni mmoja wa wabunge watano wa Reupblican wanaosema hawatamuunga mkono McCarthy.
Ameiambia televisheni ya Marekani ya Fox News kuwa hatompigia kura McCarthy kwa sababu ni sehemu ya tatizo na wala sio sehemu ya suluhisho. Amesema haoni chochote kinachoashiria kuwa McCarthy atabaubadilisha muundo tangu amekuwa katika uongozi,
Huku Warepuiblican wakiwa na wingi mchache wa viti 222 dhidi ya 213, McCarthy anaweza hata kupoteza viti vinne tu kutoka upande wake na kushinda kura 218 anazohitaji, au zaidi ya nusu ya wabunge 435 wa baraza hilo la wawakilishi
Hakuna Wademocrat wanaotarajiwa kumpigia kura. Lakini baadhi ya wabunge katika chama cha McCarthy wamependekeza kuwashawishi wenzao wa upande wa pili kumuunga mkono mgombea wa Republican ambaye hajatambuliwa, kama wajumbe wenye msimamo mkali watakataa kulegeza upinzani wao.
Alipoulizwa na waandishi Habari kama ana kura anazohitaji, McCarthy alisema na hapa namnukuu "nadhani tutakuwa na siku nzuri kesho”. Kisha akafanya mikutano na wapinzani na wafuasi.
Warepublican wanatarajiwa kukutana ana kwa ana katika mkutano wa faragha leo asubuhi, masaa kadhaa kabla ya uchaguzi wa spika.
Spika ataweka ajenda ya bunge katika kipindi cha serikali iliyogawika mjini Washington, huku Wademocrat wa Rais Joe Biden wakisalia na udhibiti wa Ikulu ya White House na Baraza la Seneti. Ushindani wa madaraka huenda ukadhoofisha matumaini ya wabunge wa Republican ya kusonga mbele haraka na uchunguzi kuhusu utawala wa Biden na familia.
Reuters, afpe