Wabunge Marekani wafikia makubaliano ufadhili wa ukuta
12 Februari 2019Rais Donald Trump ameendelea kushinikiza azma yake ya kisiasa ya ujenzi wa ukuta katika mpaka na Mexico wakati alipofanya mkutano wa hadhara kwenye mji wa El Paso jana Jumatatu, huku wabunge mjini Washington wakisema wamefikia maridhiano ili kuepuka kufungwa tena kwa shughuli za serikali.
Kundi la maseneta wa Republican na Democrats mjini Washington wamesema kuwa wamefikia makubaliano katika
ufadhili wa serikali kuelekea tarehe ya mwisho inayotishia kufungwa tena kwa sehemu ya shughuli za serikali.
Wabunge wanakabiliwa na tarehe ya mwisho ambayo ni Februari 15 ya ufadhili wa serikali ili kutimiza matakwa ya rais Donald Trump juu ya ujenzi wa ukuta na Mexico.
Ikiwa tarehe hiyo ya mwisho itafikiwa bila muafaka, serikali huenda ikafunga sehemu fulani ya shughuli zake na kuwalazimu mamia kwa maelfu ya wafanyakazi wa shirikisho kufanya kazi bila ya malipo. Vyombo vya habari vya Marekani vimemnukuu seneta wa Republican Richard Shelby kuwa kumefikiwa makubaliano yanayojumisha dola bilioni 1.375 kufadhili ukuta mpya, licha ya kwamba Trump ameomba dola bilioni 5.7.
Trump alikubali kufadhili serikali kwa muda wa wiki tatu ili kuruhusu majadiliano baada ya muafaka kutopatikana pindi shughuli za serikali zilipositishwa kwa muda mrefu katika historia ya Marekani, na kisha zikafunguliwa Januari 25. Rais Trump anasema ukuta huo ni muhimu ili kuzuia wimbi la wahamiaji wasio na vibali, magenge ya wauza unga pamoja na biashara haramu ya usafirishaji binadamu.
Akiwahutubia maelfu ya watu katika mji huo wa El Paso Trump muda mchache baada ya tangazo la maseneta, rais huyo amesema bado hajaelezwa juu ya mpango wa ufadhili lakini akasisitiza kwamba ukuta lazima ujengwe.
"Na Hakuna sehemu nzuri ya kuzungumza juu ya usalama wa mpaka ikiwa wanapenda au la, kwa sababu nimesikia mambo mengi, 'oh ukuta hauwezi kuleta tofauti nyingi'. Mnajua wapi umeleta tofauti kubwa? hapa, hapa El Paso", alisema Trump.
Kwa mujibu wa Trump wahamiaji haramu ni kitisho kikubwa kwa usalama wa taifa na wanaweza kuzuilia kwa kupanua vizuizi vilivyopo sasa. Suala la utata wa mpaka ni mwanzo wa azma yake ya kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa 2020 na mkutano wa El Paso umetoa taswira ya masuala yanayotarajiwa.
El Paso imekuwa ni sehemu kubwa ya mikutano ya rais Trump ambaye anasema ukuta uliojengwa katika eneo hilo umepunguza kiasi kikubwa uhalifu. Lakini takwimu zinaonyesha kwamba uhalifu ulipungua kabla hata ukuta huo ujengwe mwishoni mwa 2000.
Wakati wa mkutano wake mbunge wa zamani na ambaye huenda akawa mgombea urais wa Democratic Beto O'Rourke naye aliendesha mkutano mwingine wa kumjibu Trump maeneo hayo ya karibu.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga