Senegal: Wabunge wajadili pendekezo la kuahirisha uchaguzi
5 Februari 2024Wabunge nchini Senegal wameanza kujadili pendekezo lililowasilishwa la kuuakhirisha uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari.
Bunge linatathmini waraka wa pendekezo ulioidhinishwa jana na kamati ya maandalizi ,linalotaka uchaguzi uakhirishwe kwa miezi sita au hata mwaka mmoja na kufanyika Februari mwaka 2025.
Pendekezo hilo liliwasilishwa na wafuasi wa Karim Wade ambaye jina lake liliondolewa kwenye orodha ya wagombea urais na baraza la katiba la Senegal.
Soma: Watu waandamana Senegal kupinga uamuzi wa Rais kuahirisha uchaguzi
Pendekezo hilo linasema kwamba kuakhirisha uchaguzi itakuwa hatua itakayoepusha ukosefu wa uthabiti kwenye taasisi na machafuko ya kisiasa lakini pia kuhakikisha kuandaliwa kikamilifu kwa mchakato wa uchaguzi.Pendekezo hilo limeshaungwa mkono na kambi ya rais Macky Sall bungeni.
Upande mwingine ripoti zimeeleza kwamba serikali mjini Dakar imefunga mtandao wa mawasiliano ya simu za mkononi,huku viongozi wa upinzani na wafuasi wao wakiandamana kupinga hatua ya kuakhirisha uchaguzi.