Johnson apata pigo kura ya kuzuia Brexit ya bila makubaliano
4 Septemba 2019Hatua hiyo sasa inapisha njia kwa wabunge kupitisha sheria baadae siku ya Jumatano, ambayo itamshinikiza Waziri mkuu Boris Johnson kuuomba Umoja wa Ulaya kuchelewesha tena Brexit, jambo ambalo amesema hatolifanya chini ya mazingira yoyote. Baada ya kura ya jana usiku, Johnson alisema atawasilisha muswada wa kuitisha uchaguzi wa mapema. Ili aweze kuitisha uchaguzi wa mapema, muswada huo utapaswa kupitishwa na theluthi mbili ya wabunge. Serikali ya waziri mkuu imepoteza wingi wa viti bungeni, baada ya mbunge wa Conservative Phillip Lee kuhama upande wa chama hicho na kuketi upande wa Liberal Democrats, wakati waziri mkuu alipokuwa akizungumza katika baraza la chini la bunge la Uingereza. Msemaji katika ofisi ya wazri mkuu amesema wabunge wote 21 waasi wa Conservative walioipinga serikali ya Johnson watafukuzwa ndani ya chama.