1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Ethiopia wamchagua rais mpya wa awamu ya tano

8 Oktoba 2024

Wabunge wa Ethiopia wamemchagua hapo jana Waziri wa Mambo ya Nje Taye Atske Selassie kuwa rais mpya wa nchi hiyo na hivyo kuiacha Afrika ikiwa na rais mmoja tu mwanamke ambaye ni Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Ethiopia Taye Atske-Selassie Amde
Rais Taye Atske-Selassie Amde ahutubia kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wakati huo akiwa waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia , Septemba 27, 2024.Picha: Pamela Smith/AP/picture alliance

Atske Selassie mwenye umri wa miaka 68, anakuwa rais wa awamu ya tano tangu Ethiopia ilipopitisha katiba yake ya sasa mnamo mwaka 1995. Ataweza kushikilia wadhifa huo kwa muda usiozidi mihula miwili ya miaka sita.Rais huyo anachukua nafasi ya Sahle-Work Zewde mwenye umri wa miaka 74 na mwanadiplomasia anayeheshimika ambaye alihudumu kama rais tangu 2018 muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuingia madarakani mwaka 2018. Uteuzi wake ulisaidia kuimarisha sifa za Abiy kwa serikali za Magharibi, pamoja na mageuzi yake ya kiuchumi, uteuzi wa baraza la mawaziri lenye usawa wa kijinsia na mkataba wa amani na Eritrea ambao ulimwezesha kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel.Lakini vita vya kikatili dhidi ya waasi katika eneo la Tigray kati ya mwaka 2020 na 2022 na migogoro inayoendelea dhidi ya makabila mengine vimeharibu mno hadhi yake ya kimataifa.