1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge Kenya wagawika kuhusu utekelezaji wa ripoti ya BBI

Shisia Wasilwa
2 Desemba 2019

Siku chache baada ya kuzinduliwa kwa ripoti ya Maridhiano maarufu BBI, nchini Kenya, wabunge wamegawanyika kuhusu utekelezaji wake.

Kenia Building Bridges Initiative (BBI)
Picha: AFP/T. Karumba

Waasisi wakuu wa Ripoti ya BBI, rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga walitarajia kuwa matokeo yake yangeleta mshikamano wa taifa na kuondoa misuguano ya kisiasa na kikabila. Hata kabla ya maoni ya wananchi kusikizwa, ripoti hiyo yaelekea kuwagawanya wanasiasa zaidi badala ya kuwaunganisha.

Walipokongamana katika ukumbi wa Bomas, viongozi walionekana kuzungumza lugha ya umoja, lakini wikendi hii, kikundi cha wabunge 57 wa Mlima Kenya anakotokea rais Kenyatta wameapa kuipinga kura ya maoni wakisema kuwa ni ghali mno kwa mlipa kodi. Taifa litahitaji shilingi bilioni 20 kuandaa kura ya maoni. Fedha nyingine kama hizo zilitumika kuandaa ripoti yenyewe.

Msimamo wao unakwenda kinyume na azma ya rais Kenyatta na Raila wanaotaka wananchi wahusishwe. Seneta Njeru Ndwiga alisoma mwafaka huo.

"Tunashikilia kuwa marekebisho yoyote ambayo yatafanywa kwa ripoti ya BBI, yanafaa kuongozwa na bunge. Tayari watu wetu wana mizigo mingi hivyo hawafai kuwekewa mzigo mwingine wa kura ya maoni," alisema Seneta Njeru.

Viongozi hao wanahoji kuwa bunge lina uwezo wa kuyafanyia marekebisho mapendekezo hayo bila ya kuwahusisha wananchi. Hali ya wasiwasi inazidi kulikumba eneo hilo la Mlima Kenya, huku rais Uhuru Kenyatta akinyamazia suala la urithi, baadhi ya viongozi wakielezea kutoridhika kwao na jinsi rais, anavyomdhalilisha makamu wake.

Spika wa bunge avunja matarajio ya kundi linamuunga mkono makamu wa rais wa Kenya

Bunge la Kenya Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Lakini ni matamshi ya spika wa bunge Justin Muturi ambayo yanavunja matarajio ya kundi linaloegemea upande wa makamu wa rais William Ruto linalotaka ripoti hiyo ijadiliwe bungeni badala ya kuwahusisha wananchi.

Kinachosikitisha ni kuwa viongozi ambao wamejitokeza wazi kuelezea misimamo yao, hawajaonekana wakitoa hamasisho kwa wananchi kuhusu ripoti ya BBI, lakini wanaonekana kupigania maslahi yao binafsi kwenye majukwaa ya kisiasa.

Kwa viongozi wa chama tawala cha Jubilee ripoti ya BBI inalenga kumsaidia rais Uhuru Kenyatta kumfanya Raila Odinga kusalia mamlakani baada ya kukamilisha utawala wake wa mihula miwili. Aden Duale ni Kiongozi wa chama cha Jubilee chenye wabunge wengi bungeni.

"Nataka Raila aambie wakenya kwamba ile BBI na matarajio yake, amekosa yote, lazima akubali amepigwa chenga,” alisema Aden Duale

Upande unaogemea Raila unataka nafasi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka kinyume na ilivyopendekezwa kwenye ripoti hiyo, ambapo atakuwa akichaguliwa na rais na anaweza akafutwa kazi wakati wowote na rais.

Shisia Wasilwa, DW Nairobi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW