Wabunge wa Marekani kupigia kura makubaliano ya mzozo wa madeni
1 Agosti 2011Zikiwa zimesalia siku mbili tu kabla Marekani kupungukiwa na fedha katika hazina yake, rais Obama alitangaza jana jioni baada ya mazungumzo yaliyodumu muda mrefu na mahasimu wake wanasiasa wa chama cha Republican, kwamba wamefikia makubaliano ya kupunguza matumizi kwa kima cha dola trilioni 2.4.
"Viongozi wa vyama vyote viwili katika baraza la wawakilishi na seneti wamefikia makubalianio. Siyo niliyoyataka na kazi bado ipo. Nawahimiza viongozi wa vyama vyote waunge mkono muswada huu kwa kura zao katika siku chache zijazo."
Hali ya kutoridhika
Hali ya kutoridhika imejitokeza huku barala la seneti linalodhibitiwa na chama cha Democratic cha rais Obama likitarajiwa kuyaridhia makubaliano hayo yanayoongeza uwezo wa Marekani kukopa fedha na kupunguza takriban dola trilioni 2.4 kutoka kwa nakisi iliyopo katika muongo mmoja ujao. Hata hivyo upinzani mkali unatarajiwa katika baraza la wawakilishi ambamo wafuasi wa chama cha kihafidhina cha Tea Party na wabunge wa kiliberali wameelezea kutoridhika kwao juu ya makubaliano yaliyofikiwa.
Kiongozi wa chama cha Democratic katika baraza la seneti, Harry Reid, amesema, "Hakuna upande uliopata ulichokitaka katika makubaliano haya. Hivyo ndivyo ilivyo katika makubaliano."
Huku makubaliano hayo yakifikiwa dakika ya mwisho ili kuiepusha Marekani kutokana na kushindwa kulipa madeni yake, viongozi wa serikali na wawekezaji watafuatilia kwa karibu kuona ikiwa yatakwenda mbali kuyashawishi mashirika yanayoweka viwango vya mikopo kuicha Marekani iendelee kuhifadhi kiwango chake cha kukopa fedha. Shirika la Standard and Poor lilionya lingepunguza uwezo wa Marekani kukopa fedha kama viongozi hawangefikia makubaliano.
Makubaliano yapongezwa
Waziri wa fedha wa Ufaransa Francois Baroin ameyapongeza makubaliano yaliyofikiwa akisema ni hatua inayoelekea mkondo wa sawa wa kuimarisha ukuaji wa uchumi wa dunia. Kwa upande mwingine thamani ya hisa za Japan imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 1 leo Jumatatu huku masoko ya uuzaji wa mafuta yakiimarika kufuatia tangazo la rais Obama.
Mpango huo ni mchakato unaojumuisha hatua mbili za kupunguza deni la Marekani. Hatua ya kwanza inataka matumizi yapunguzwe kwa kima cha dola bilioni 900 katika muongo mmoja ujao na ya pili inataka kutafutwe njia ya kuhifadhi dola trilioni 1.5 na kamati maalumu ya bunge. Bunge linalazimika kuyatekeleza makubaliano hayo kufikia Desemba 23 mwaka huu.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE
Mhariri: Abdul-Rahman, Mohamed