1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Somalia kumchagua rais mpya

8 Februari 2017

Wabunge na maseneta wa Somalia leo wanamchagua rais wa nchi hiyo, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa. Uchaguzi huo unafanyika baada ya kuahirishwa kwa miezi kadhaa na kutokana na kitisho cha Al-Shabaab.

Somalia Wahlen - Plakate in Mogadischu
Picha: picture-alliance/abaca/S. Mohamed

Wabunge na maseneta hao wamekusanyika nyuma ya majengo ya uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kwa ajili ya kukamilisha zoezi la kumchagua rais wa nchi hiyo. Uchaguzi huo wa muda mrefu ulianza kwa kuwachagua wazee na watu maarufu wa kikanda 14,000, kuwachagua wabunge 275 na maseneta 54, ambao sasa ndiyo wataamua iwapo wamuunge mkono Rais Sheikh Mohamud kwa mara ya pili au kumchagua mmoja kati ya wapinzani wake 21.

Ulinzi mkali umeimarishwa mjini Mogadishu kutokana na hofu ya mashambulizi ya wanamgambo wa Al-Shabaab, ambao walitishia kuvuruga mchakato mzima wa uchaguzi. Uwanja wa ndege wa Mogadishu pamoja na barabara zote kuu za mji huo zimefungwa.

Rais wa Somalia aliyeko madarakani Hassan Sheikh MohamudPicha: Reuters/M. Dalder

Uchaguzi huo ambao awali ulipangwa kufanyika mwezi Agosti, unatarajiwa kuanza mchana huu na inaripotiwa kwamba unaweza ukachukua duru kadhaa kabla ya mshindi kutangazwa. Uwanja huo wa ndege unalindwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika, AMISOM. Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na balozi za kigeni ziko katika eneo hilo.

Mwangalizi wa uchaguzi huo na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Mohamed Shire, anasema ni jambo jema kwamba uchaguzi huo sasa unafanyika na hiyo ni hatua kubwa kwa wananchi wa Somalia, kwani pia jumuiya ya kimataifa imekuwa ikionyesha kuunga mkono mchakato mzima wa uchaguzi.

Matokeo yanasubiriwa kwa hamu

''Kila mmoja anangoja kuona kile kitakachojiri, matokeo ya uchaguzi huu. Kuna wagombea wakuu wanne hapa. Rais aliyeko madarakani, Hassan Sheikh Mohamud, Waziri Mkuu aliyeko madarakani, Omar Abdirashid Ali Sharmake. Pia yuko rais wa zamani, Sharif Sheikh Ahmed, lakini pia waziri mkuu wa zamani, Farmaajo,'' alisema Shire.

Wagombea hao wa urais wamekuwa wakishutumiana wenyewe kwa wenyewe kwa kuwanunua wabunge kadhaa waaminifu, ingawa shutuma hizo zimakanushwa. Kundi la kupambana na rushwa la Marqaati limesema maelfu ya Dola zimekabidhiwa kwa watu binafsi kwa ajili ya kujihakikishia ushindi katika uchaguzi huo.

Wanajeshi wa AMISOM wakifanya doria mjini MogadishuPicha: picture-alliance /dpa/F. Abdi Warsameh

Mwishoni mwa juma lililopita, wagombea hao walilihutubia bunge, huku rais aliyeko madarakani akisema anahitaji miaka mingine minne kwa ajili ya kuimarisha zaidi usalama na uchumi wa nchi hiyo, lakini wapinzani wake wamemkosoa kwa utendaji mbovu.

Uchaguzi huo ni muhimu kwa taifa hilo la Pembe ya Afrika ambayo ilitumbukia katika machafuko kutokana na kuanguka kwa utawala wa kidikteta wa Mohamed Siad Barre, mwaka 1991. Tangu wakati huo Somalia haijawahi kuwa na serikali kuu inayofanya majukumu yake vizuri, ingawa imekuwa ikijitahidi haua kwa hatua kuiamrisha demokrasia yake.

Hayo yanajiri wakati ambapo mapema leo asubuhi kundi wanamgambo wanaodaiwa kuwa wa Al-Shabaab limeshambulia katika hoteli moja kwenye mji wa bandari wa Bosaso ulioko kaskazini mwa Somalia. Watu sita wameuawa katika shambulizi la hoteli hiyo ambayo mara nyingi hukaliwa zaidi na maafisa wa Somalia pamoja na raia wa kigeni.

Duru za kiusalama zinaeleza kuwa wanamgambo kadhaa wamekamatwa. Miongoni mwa waliouawa ni wanamgambo wawili. Hadi sasa hakuna kundi lolote ambalo limekiri kuhusika na shambulizi hilo lililotokea kwenye mkoa wa Puntland wenye mamlaka yake ya ndani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA, Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf