1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras kutemea kura za upande wa upinzani

22 Julai 2015

Wabunge wa Ugiriki wameanza mjadala kuhusu mageuzi ziada yanayotakiwa na wafadhili wa kimataifa ili nchi hiyo ipatiwe mkopo mwengine. Kura inayotarajiwa baadaye leo usiku inaweza kuitia hatarini serikali ya muungano .

Bunge la Ugiriki mjini AthensPicha: picture-alliance/dpa/Robert Geiss

Kura itakayopigwa baadae kuhusu mageuzi katika sekta ya sheria na mfumo wa benki ni miongoni mwa masharti yaliyotolewa na wafadhili wa Ugiriki katika Umoja wa ulaya ili badala yake yaanzishwe majadiliano ya kupatiwa fungu la tatu la mkopo wenye thamani ya Euro bilioni 85.

Baada ya kupoteza uungaji mkono wa wabunge wengi wa chama chake katika zoezi la kuzipigia kura hatua kali za kufunga mkaja wiki iliyopita,waziri mkuu Alexis Tsipras anabidi ategemee uungaji mkono wa vyama vya upinzani vinavyoelemea upande wa Ulaya ili kupata ridhaa ya bunge.

Majadiliano pamoja na wafadhili yanatarajiwa kuanza baada ya kura hiyo ya bunge.Serikali ya Ugiriki inataraji kukamilisha mazungumzo hayo kabla ya Agosti 20,pale Ugiriki itakapolazimika kuilipa benki kuu ya Ulaya deni lenye thamani ya Euro zaidi ya bilioni 3.

Hatua zinazotakiwa na wafadhili kwaajili ya kupatiwa mkopo zimezusha fadhaa miongoni mwa wafuasi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha Alexis Tsipras.Wengi,akiwemo pia waziri wa zamani wa fedha Yanis Varoufakis walipiga kura dhidi ya hatua za kufunga mkaja wiki iliyopita.Pindi wabunge wengine wakiamua kupiga kura dhidi ya hatua hizo baadae hii leo,serikali ya Tsipras inaweza kuingia hatarini.

Maandamano dhidi ya hatua za kufunga mkaja yafanyika kabla ya kura bungeni

Wafuasi wa jadi wa chama hicho ndani ya vuguvugu linalopigania masilahi ya wafanyakazi nao pia wamehamakishwa na kile wanachokitaja kuwa "kuendewa kinyume na Tsipras jukumu walilotwikwa na wapiga kura.

Waziri mkuu Alexis TsiprasPicha: picture-alliance/AA/abaca/A. Mehmet

Muungano wa wafanyakazi wa mashirika ya umma wanapanga kuitisha maandamano dhidi ya serikali nje ya bunge,kabla ya zoezi la kupiga kura linalotegemewa milango ya saa tano usiku kwa saa za Afrika mashariki.

Tsipras amewalaumu wanaomkosoa kwa kutowajibika."Nimeona mengi na kusikia taarifa za kijasiri,lakini hadi wakati huu sikusikia pendekezo lolote mbadala" amesema waziri mkuu Alexis Tsipras mbele ya wabunge -kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi ya juu serikalini ambae hakutaka jina lake litajwe.

Alexis Tsipras amesema pia wale wanaounga mkono Ugiriki itoke katika kanda ya Euro wanabidi wajitokoeze na kusema hadharani badala ya kunong'ona kichini chini."

Mageuzi kuhusu malipo ya uzeeni ytajadiliwa baadae

Hatua za mageuzi zinazojadiliwa zinahusu mageuzi katika vyombo vya sheria na kufuatwa muongozo wa Umoja wa Ulaya katika shughuli za benki.

Maandamano ya wiki iliyopita dhidi ya hatua za kufunga mkajaPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Waziri wa fedha wa Ugiriki Euclid Tsakalotos amesema mpango wa kupunguza gharama za malipo ya uzeeni unahitaji udurusiwe kabla ya kufikishwa bungeni kwa majadiliano.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AP

Mhariri:Josephat Charo