1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Uingereza kupiga kura ya kutokuwa na imani na May

Caro Robi
12 Desemba 2018

Wabunge wa chama cha Conservative wamewasilisha hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri mkuu Theresa May, wakipinga uongozi wake kuhusiana na suala la mchakato wa Uingereza kutaka kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.

Theresa May
Picha: Reuters/P. Nicholls

Graham Brady ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Conservative bungeni amesema zaidi ya asilimia 15 ya wabunge wa chama hicho wamemuandikia barua ya kutaka kuwepo kura ya kutokuwa na imani na May.

Kura hiyo itafanyika bungeni leo kati ya saa kumi na mbili na saa mbili jioni na matokeo yake kutangazwa muda mfupi baadaye. May anaweza kuondolewa madarakani iwapo wabunge 158 kati ya 315 wa chama chake wataunga mkono kura hiyo ya kutokuwa na imani naye.

May aapa kupigana hadi dakika ya mwisho

Akipoteza kura hiyo inayopigwa leo jioni sharti aondoke madarakani lakini iwapo atashinda basi hawezi kupingwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/S. Gallup

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi yake, May amesema atapinga kura hiyo ya kutokuwa na imani naye na kila alichonacho, akiongeza kubadilisha uongozi sasa kutauweka mustakabali wa siku za usoni mwa Uingereza na majadiliano kuhusu Brexit katika hatari.

Mwenyekiti wa chama cha Labour bungeni Ian Lavery amesema mivutano ndani ya chama cha Conservative kunaziweka ajira na maisha ya Waingereza katika hatari na kuongeza udhaifu wa May kunaikwamisha serikali katika kipindi muhimu kwa taifa hilo. Wengi wa wabunge wameghadhabishwa na jinsi anavyoshughulikia mchakato wa Brexit.

Je, Uingereza itasalia EU au itajiengua?

Waziri huyo mkuu wa Uingereza jana alifanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa Umoja wa Ulaya lakini alikosa kufikia mageuzi ya rasimu ya makubaliano aliyoyafikia na Umoja wa Ulaya.

May akiwa bungeni kueleza mpango wake kuhusu BrexitPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Duffy

Waziri wa sheria David Gauke amesema Uingereza itahitaji kuchelewesha mchakato wa kujiondoa Umoja wa Ulaya iwapo May atashindwa bungeni.

Huku ikiwa imesalia chini ya miezi minne kabla ya Uingereza kuondoka rasmi kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, taifa hilo la tano imara zaidi kiuchumi duniani linakabiliwa na mzozo, kukiwa na hofu huenda ikajiengua bila ya makubaliano yoyote na hivyo kutumbukia katika mzozo mbaya wa kiuchumi au kubatilisha uamuzi wake wa kujiondoa kupitia kura nyingine ya maoni kuamua hilo.

Suala la Brexit ndiyo uamuzi mkubwa zaidi kuchukuliwa na Uingereza tangu kumalizika kwa vita vya pili vikuu vya dunia na wanaounga mkono mshikamano wa Umoja wa Ulaya wanahofia huenda suala hilo likazigawanya nchi za Magharibi wakati ambapo pia zinakabiliana na uongozi usiotabirika wa Rais wa Marekani Donald Trump, ubabe wa Urusi na nguvu za kiuchumi za China.

 

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW