1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa upinzani wajiuzulu Hong Kong

11 Novemba 2020

Wabunge 15 wanaotetea demokrasia Hong Kong wamejiuzulu, wakipinga hatua ya wabunge wengine wanne kufukuzwa, hatua inayolifanya bunge kukosa upinzani wa kutosha.

Hongkong PK Kenneth Leung, Dennis Kwok, Wu Chi-wai, Alvin Yeung und Kwok Ka-ki
Picha: Tyrone Siu/REUTERS

Mapema Jumatano uongozi wa Hong Kong uliwafukuza wabunge wanne kwa sababu za "usalama wa kitaifa" bila kuwafikisha mahakamani na bila kutoa taarifa zaidi. Sheria mpya inauruhusu uongozi wa mji huo kuwafukuza wabunge bila ya kuwapeleka mahakamani, baada ya China kuuidhinisha muswada huo mpya.

Wabunge hao walikuwa kundi la mwisho la wanasiasa wanaotetea demokrasia. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya China kuidhinisha muswada unaoruhusu serikali kuwafukuza.

Wabunge wanaweza kufukuzwa iwapo wataonekana kuwa hatari kwa usalama wa taifa, kama wanataka uhuru wa mji huo, kama watakataa kukubali China kuwa na mamlaka juu ya Hong Kong, au kama watatafuta msaada wa kigeni.

Sheria hiyo ilipitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge la Watu wa China, iliyokutana Jumanne na Jumatano. Wabunge wa upinzani katika bunge hilo lenye viti 70 walitishia kujiuzulu kwa wingi iwapo mbunge yeyote anayetetea demokrasia atafukuzwa kutoka kwenye baraza hilo la kutunga sheria. Soma zaidi  Bunge la China lapitisha pendekezo la kutungwa sheria ya usalama

Akizungumza na waandishi habari wakati akitangaza hatua yao ya kujiuzulu, kiongozi wa kambi ya upinzani, Wu Chui-wai amesema wanajiuzulu katika nafasi zao, kwa sababu wenzao wamefukuzwa na serikali kuu isiyo na huruma.

"Leo tunatangaza kujizulu kwa wingi na barua zetu za kujiuzulu zitawasilishwa kesho kwa Spika wa Baraza la Kutunga Sheria, Legco. Na tuna matumaini kwamba kila mmoja ataona," alifafanua Wu.

Wu amesema ingawa wanakabiliana na changamoto nyingi katika siku zijazo za kupigania demokrasia, lakini kamwe hawatokata tamaa.

Wabunge waliofukuzwa ni pamoja na Alvin Yeung, Dennis Kwok, Kwok Ka-ki na Kenneth Leung. Awali wabunge hao walizuiwa kugombea tena katika uchaguzi wa bunge, kutokana na maafisa kugundua kwamba ahadi yao ya utii kwa Hong Kong haikuwa ya kweli.

Hiyo ilikuwa kabla ya uchaguzi kucheleweshwa kutokana na janga la virusi vya corona.

Heshima ya kutetea demokrasia 

Wabunge wa Hongkong Carrie Lam, Dennis Kwok, Kenneth Leung, Kwok Ka-ki, Alvin YeungPicha: Vincent Yu/AP Photo/picture alliance

 

Dennis Kwok amewaambia waandishi habari kwamba imekuwa heshima kubwa kwao kufukuzwa kwa sababu ya kupigania demokrasia. Amesema kwa upande wa uhalali na katiba, ni wazi kwa maoni yao kwamba uamuzi huo umekiuka sheria ya msingi na haki zao za kushiriki katika masuala ya umma.

Kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam amesema hatua ya kufukuzwa wabunge hao imefanyika kwa kuzingatia "katiba, sheria, busara na ulikuwa muhimu".

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International imeikosoa sheria hiyo mpya likisema ni mfano wa kampeni nyingine ya serikali kuu ya China kuwanyamazisha wapinzani wa Hong Kong kwa namna yoyote ile.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo kanda ya Asia-Pasifiki, Yamini Mishra amesema kwa mara nyingine tena Hong Kong imeruhusu sheria zake na bunge kuingiliwa, huku serikali ya China ikifanya maamuzi holela yanayodhihaki utawala wa sheria.

 

 

(AP, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi

Gundua zaidi