1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wamegawika kuhusiana na Johnson

6 Juni 2022

Wabunge wa chama tawala cha Kihafidhina nchini Uingereza wamegawika kuhusiana na iwapo Waziri Mkuu Boris Johnson anastahili kuendelea kuwa kiongozi wao.

Boris Johnson UK Premierminister
Picha: James Veysey / Avalon/picture alliance

Hii ni kufuatia tangazo kwamba barua za kutosha za kuanzisha mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye zimewasilishwa kwa mkuu wa chama hicho hivyo kupelekea kura ya maoni kufanyika baadae Jumatatu.

Baadhi ya wabunge wa chama hicho cha Kihafidhina wanasema Johnson ni mlaghai na hawezi kuiongoza nchi baada ya kuzongwa na sakata chungunzima.

Mbunge John Penrose ametangaza amejiuzulu kama kiongozi wa kukabiliana na ufisadi nchini humo, akisema ripoti ya mchunguzi wa utumishi wa umma Sue Gray kuhusu mikusanyiko ya kinyume cha sheria katika makao na afisi ya waziri mkuu nambari 10 Downing Street wakati wa vikwazo vya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, ni jambo linaloonyesha kwamba Waziri Mkuu huyo amevunja maadili ya mawaziri na anastahili kuachia ngazi.

Baadhi ya wabunge wanatarajia ashinde kura ya kutokuwa na imani

"Kimsingi kura moja ya wingi inatosha usiku wa leo. Tatizo ni iwapo ataponea au la wakati ana tatizo lan kiungozi linalomkabili. Lakini matokeo yako wazi kabisa kwamba yeyote anayeshinda kwa wingi mdogo hatodumu kwa muda mrefu baada ya hapo," alisema Penrose.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akiwa bungeniPicha: various sources/AFP

Wabunge wengine katika chama hicho wanatarajia aishinde kura hiyo ingawa amepitia kadhia nyingi za kisiasa. Baadhi ya hao wabunge wanaamini kwamba huenda baada ya kura hiyo akaipanga upya serikali yake na kufuata kanuni za Kihafidhina.

Waziri wa fedha Rishi Sunak ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba anamuunga mkono Johnson katika kura ya Jumatatu. Na katika barua walizotumiwa wabunge wa chama hicho Jumatatu, Johnson mwenyewe amehimiza hoja hiyo hiyo ya kutaka wamuunge mkono.

Jacob-Rees Mogg ni mbunge aliyekuwa anaunga mkono mchakato wa Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit, ambao Johnson aliukamilisha na anasema waziri mkuu huyo ni kiongozi shupavu aliyepewa idhini ya uongozi na Waingereza. Mogg anasema wale wanaompinga wanafanya hivyo kwa kuwa hawakubaliani na matokeo ya Brexit.

Gharama ya juu ya maisha inawazonga Waingereza

"Walifikiri Waingereza walikosea. Walifikiri Waingereza walikosea kwa kumpa Waziri Mkuu idhini ya uongozi. Nafikiri Waingereza walikuwa sahihi na tunastahili kumuunga mkono Boris Johnson na mamlaka aliyo nayo," alisema Mogg.

Afisi na makao ya Waziri Mkuu wa Uingereza nambari "10 Downing Street"Picha: David Cliff/NurPhoto/imago images

Waziri Mkuu Johnson au yule atakayeichukua nafasi yake, wanakabiliwa na matatizo mengi miongoni mwao ikiwa gharama ya juu zaidi ya maisha inayowakabili Waingereza, wakati ambapo bei ya chakula na mafuta ikiwa inapanda na mishahara ikiwa imesalia pale pale.

Iwapo atashindwa kura hiyo ya kutokuwa na imani naye, waziri wa zamani wa afya Jeremy Hunt ndiye aliye katika mstari wa mbele katika wale wanaotarajiwa kuichukua nafasi ya Johnson akifuatiwa na waziri wa zamani wa mambo ya nje Liz Truss.

Chanzo: Reuters/APE