Wabunge waridhia mjadala wa kumuondoa makamu rais Kenya
2 Oktoba 2024Gachagua anatuhumiwa kwa kuihujumu serikali, kuhusika katika ufisadi, ukaidi, kuendesha siasa za migawanyiko ya kikabila miongoni mwa mashitaka mengine kadhaa.
Wabunge kiasi 291 walitia saini kuunga mkono hoja iliyowasilishwa bungeni, ikiwa ni zaidi ya idadi ya chini ya wabunge 117 inayotakikana kuruhusu mjadala huo.
Spika wa bunge la kitaifa, Moses Wetangula, alisema hoja hiyo iliyowasilishwa na Mutuse Eckomas Mwengi, mbunge kutoka muungano unaotawala, iliafiki viwango vyote vya kikatiba vinavyohitajika.
Soma zaidi: Bunge la Kenya lapokea hoja ya kuuzuliwa makamu wa rais
Hoja hiyo inaorodhesha sababu 11 za kumshitaki Gachagua, ikiwa ni pamoja na kujikusanyia utajiri unaokadiriwa kuwa shilingi bilioni 5.2 katika kipindi cha miaka miwili dhidi ya mshahara wake wa jumla ya dola 93,000 kila mwaka.
Ili hoja hii ipitishwe, inahitaji kuungwa mkono na angalau theluthi mbili ya wabunge wa bunge la taifa.
Mjadala na kura inatarajiwa kufanyika Jumanne ijayo kabla kuelekea katika baraza la seneti.