1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wazuia Uingereza kuondoka EU bila makubaliano

14 Machi 2019

Wabunge wa Uingereza wamepiga kura kuizuia nchi hiyo kuondoka katika Umoja wa Ulaya bila ya kufikiwa makubaliano ya aina yoyote.

London: Brexit Proteste am 12. März
Picha: picture-alliance/Zumapress

 Wabunge 321 wamepiga kura kuipinga hatua hiyo, huku 278 wakiunga mkono Uingereza kuondoka kwenye umoja huo kiholela. Kura ya jana imepigwa baada ya ile ya Jumanne, ambapo wabunge waliukataa mpango wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kuhusu masharti ya nchi hiyo kuachana na Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit.

Hatua ya Uingereza kuondoka bila ya makubaliano kuhusu uhusiano wa baadae kati ya pande hizo mbili, ingesababisha hatari kubwa katika biashara na mustakabali wa watu wa Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Kura nyingine kupigwa leo

Kinachofuata kwa sasa ni kura itakayopigwa leo na wabunge wa Uingereza kuamua iwapo wauombe Umoja wa Ulaya kuuchelewesha muda wa Brexit wa Machi 29, uliokuwa umepangwa awali kisheria. Hata hivyo, suala la kuongeza muda wa Brexit linahitaji kuidhinishwa na nchi zote 27 wanachana wa Umoja wa Ulaya. Ombi hilo la Uingereza linaweza kujibiwa katika mkutano wa kilele wa umoja huo uliopangwa kufanyika Machi 21 na 22.

Serikali ya May imesema itapendekeza kura ya tatu bungeni kuhusu mpango wa Brexit ifanyike Machi 20 kabla ya mkutano huo wa kilele. Iwapo wabunge wa Uingereza wataukataa tena mpango huo, May amesema ataomba mchakato wa Brexit ucheleweshwe hadi Juni 30. Amesema wabunge wameonesha msimamo wao kwa kiasi kikubwa kupinga kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya kiholela, lakini sasa wanapaswa kufanya kazi kuhakikisha wanapata ufumbuzi.

Theresa May (katikati) akifatilia kura bungeniPicha: picture-alliance/AP/M. Duffy

Aidha, May amesema bila shaka Baraza la Umoja wa Ulaya halitoweza kuongeza muda bila ya kuwa na kusudio la wazi na kwamba hatua yoyote ya kuchelewesha Brexit, itaibidi Uingereza kushiriki katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya mwezi May, hata kama inajiandaa kuondoka. Baada ya Brexit, Uingereza haitawakilishwa katika Bunge la Ulaya na nafasi yake imeshazibwa na nchi nyingine.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema ombi la kuchelewesha muda wa Brexit litafikiriwa, lakini sio moja kwa moja. Macron amesema serikali ya Uingereza inahitaji kuueleza Umoja wa Ulaya kuhusu suala hilo na hasa kama litakuwa na mantiki.

Umoja wa Ulaya wazungumza

Mwakilishi wa bunge la Umoja wa Ulaya anayesimamia mchakato wa Brexit, Guy Verhofstadt, amesema anapinga hatua yoyote ya kuongeza muda wa Brexit, iwe ni kwa siku moja, wiki moja au hata saa 24, kama haitokani na kile kilichofikiwa na wabunge wa Uingereza. Ameitaka serikali ya Uingereza kuamua kuhusu Brexit, kwa sababu hali ya kutokuwa na uhakika haiwezi kuendelea.

Kiongozi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Brexit, Michel Barnier amesema Uingereza ina jukumu la kusema kile inachokitaka kwa ajili ya mustakabali wa uhusiano wa pande hizo mbili. Barnier ameliambia Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, haoni haja ya kuongeza muda wa mazungumzo.

Akizungumza baada ya matokeo ya kura ya jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amewapongeza wabunge wa Uingereza kwa kuzuia kuondoka kiholela bila makubaliano.

Maas ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba hatua ya Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya bila makubaliano haina maslahi yoyote kwa pande hizo mbili na siku zote wamekuwa wakiliweka hilo wazi. Amesema ni muda sasa kwa Uingereza kueleza kile inachokitaka ili kuufanikisha mpango wa Brexit, kwa sababu muda unakimbia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW