1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachache wajitokeza kujisajili uchaguzi wa mitaa Tanzania

11 Oktoba 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Ijumaa aliwaongoza Watanzania kujiandikisha katika daftari la wapiga kura la uchaguzi wa serikali za mitaa.

Tansania Sansibar Präsidentin Samia Suluhu Hassan bei Kizimkazi Festival
Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: Presidential Press Service Tanzania

Haya ni maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu, huku kukiwa na mwamko mdogo wa wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika daftari hilo.

Akizungumza Ijumaa mara baada ya kujiandikisha katika kitongoji cha Sokoine, wilayani Chamwino, Dodoma, Rais Samia aliwasisitiza Watanzania kujitokeza kujiandikisha kwani uchaguzi huu ndio unaotoa taswira ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Mwamko mdogo wa kujiandikisha

Rais Samia, alitumia fursa hiyo kuikumbusha jamii kufanya zoezi hili kwa usalama na amani na kuchagua viongozi wenye sifa, bila upendeleo na bila kujali jinsia.

Raia wa Tanzania akishiriki zoezi la uchaguziPicha: Reuters

Hata hivyo, wakati zoezi hilo likiendelea, kulikuwa na mwamko mdogo wa wananchi kujiandikisha katika baadhi ya maeneo ya mikoani na mjini Dar es Salaam kwa kile kinachoelezwa kuwa zoezi hilo limeangukia wakati wa siku ya kazi na wengine wakisema wananchi hawakupewa taarifa za kutosha kuhusu zoezi hilo.

Aidha, kwa upande wa mikoa mingine ya Tanzania, Mwenyekiti wa kijiji cha Chikunja, wilayani Masasi katika mkoa wa Mtwara, John Kamtaule aliiambia DW kuwa mwamko bado ni mdogo kwa watu wanaojitokeza kujiandikisha.

Navyo vyama vya siasa Tanzania viliibua malalamiko vikidai kuwa zoezi la uandikishaji  lina mapungufu hasa katika utolewaji wa taarifa.

ACT Wazalendo chakosoa utoaji wa taarifa za kujiandikisha

Alhamis Chama cha Upinzani Tanzania ACT-Wazalendo kupitia Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu kilisema vyama hivyo vilipewa taarifa juzi Oktoba 9 ya kupeleka orodha ya mawakala na kusema kuna udhaifu mkubwa katika upatikanaji wa mawakala wa vyama vya siasa.

Wanachama wa chama cha ACT WazalendoPicha: Office of the First Vice President of Zanzibar

Pamoja na Rais Samia kuongoza zoezi rasmi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura akiwa Dodoma, kadhalika baadhi ya viongozi akiwamo Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko, ambaye yeye aliongoza kujiandikisha katika wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, walishiriki zoezi hilo.

Wengine ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dorothy Gwajima ambaye alijiandikisha katika eneo la Salasala, Dar es Salaam.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW