1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachache wajitokeza kupiga kura Nakuru

9 Agosti 2022

Shughuli ya kupiga kura katika eneo la Nakuru inaendelea kukiwa na ripoti za matatizo kwenye makaratasi ya kura na vifaa vya kupigia kura kwenye maeneo mengine.

Kenia Nairobi Wahlen Wahllokal
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Idadi ya wapiga kura pia inaripotiwa kuwa chini ikizingatiwa na chaguzi za awali.

Milango ya vituo vya kupiga kura eneo la Rongai ilipofunguliwa mapema Jumanne, wananchi waliokuwa wamejitokeza kutimiza wajibu wao wa kupiga kura waligundua kwamba majina ya wagombea wa viti vya bunge la kitaifa kwenye eneo hilo hayakuwepo.

Eneo bunge la Rongai lipo kaunti ya Nakuru. Mmoja wa wagombea wa kiti hicho ni mbunge wa eneo hilo Raymond Moi, mtoto wa marehemu Rais wa pili wa Kenya Daniel Moi, na alikuwa amejiwasilisha kukitetea kiti chake.

Ameelezea kukerwa na sintofahamu hiyo ambayo ni kinyume na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, Wafula Chebukati kwamba maandalizi yako tayari na uchaguzi utakuwa huru.

''Nimeshangaa sana nilipojaribu kupiga kura na nikajikuta siko kwenye karatasi ya kupigia kura. Huu ni uzembe wa aina gani? Mwenyekiti alituhakikishia wako tayari, lakini hawako tayari. Jambo kama hilo limefanyika kule Kacheliba, limefanyika Pokot Magharibi,'' alifafanua Raymond.

Afisa wa uchaguzi akiweka vifaa vya uchaguzi kwenye kituo cha kuigia kuraPicha: Halima Gongo/DW

Analalamika kwamba hili litaathiri matokeo ya uchaguzi wa urais. Raymond Moi anagombea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha KANU iliyo kwenye muungano wa Azimio la Umoja, dhidi ya mpinzani wake Chebor Mamba wa chama cha UDA kinachoongozwa na naibu Rais William Ruto. Chebor vilevile ameelezea kugadhabishwa na matukio hayo.

Joseph Mele, afisa mkuu wa IEBC kaunti ya Nakuru amesema hili ni jambo linaloshughulikiwa na usimamizi wa tume hiyo ya IEBC.

Kumekuwepo pia na malalamiko ya kukosekana kwa taarifa za baadhi ya wapiga kura kwenye vifaa vya kupiga kura.

Vituo vya kupigia kura kaunti ya Nakuru vinashuhudia idadi chache ya wapiga kura hasa kati ya vijana ambao walionekana kushabikia sana mikutano ya kampeni za siasa. ''Kuna muda bado, tungependa watu wajitokeze. Kama taifa tumetumia mabilioni ya pesa kuandaa shughuli hili, kwa hiyo idadi ikiwa chache ni uharibifu mkubwa wa pesa za umma,'' alisema Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui.

Gavana Kinyanjui anakitetea kiti chake dhidi ya mpinzani wake Susana Kihika wa chama cha UDA.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW