1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUrusi

Wachezaji wa Urusi waruhusiwa katika mashindano ya Tenisi

1 Mei 2023

Daria Kasatkina amesema anashukuru kwamba wachezaji wa tenisi wa Urusi bado wana uwezo wa kushiriki mashindano ya kimataifa huku michezo mingine ikipigwa marufuku kutokana na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

 WTA Premier St Petersburg | Russische Tennisspielerin Darya Kasatkina
Mcheza tenisi wa Urusi Daria KasatkinaPicha: Alexander Demianchuk/TASS/dpa/picture alliance

"Nilihuzunika sana kukosa mashindano ya Wimbledon mwaka jana- bila shaka kutokana na sababu, japo ilikuwa uchungu,” Kasatkina amewaambia waandishi wa habari baada ya kumshinda Lesia Tsurenko, raia wa Ukraine katika mashindano ya wazi ya Madrid.

Tenisi, tofauti na michezo mingine, imekwepa shoka la marufuku kwa wachezaji kutoka Urusi na washirika wake Belarus baada ya uvamizi nchini Ukraine ambao Moscow unauita "oparesheni maalum ya kijeshi.”

Hivi karibuni, baadhi ya michezo imeanza kuwaruhusu tena wanariadha wa Urusi na Belarus kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) mwezi uliopita.

Soma pia: Muguruza na Azarenka kukwaana nusu fainali Qatar Open

Mashindano ya tenisi ya Wimbledon iliwapiga marufuku wachezaji kutoka Urusi na Belarus, japo mnamo mwezi Machi usimamizi ulisema utawaruhusu kushiriki kama wanariadha wasiogemea nchi yoyote.

"Nina furaha kwamba tutaweza kurejea tena uwanjani mwaka huu na kusema kweli, tuna bahati kwamba kama wanamichezo tunaweza kushiriki.”

Kasatkina ambaye alifuzu robo fainali ya mashindano ya Wimbledon mwaka 2018, ameongeza, "Asilimia 95 ya wanariadha kutoka Urusi hawakuweza kushiriki michuano ya kimataifa, na tunathamini sana fursa hii ya kushiriki tena na kuwepo kwenye jukwaa la kimataifa.”

Lessja Tsurenko ambaye mwaka uliopita alisema hakutaka kucheza dhidi ya wanamichezo wa Urusi au Belarus, hakusalimiana na Kasatkina baada ya mchezo wa raundi ya tatu mjini Madrid.

Soma pia: Boris Becker ana wasiwasi kuhusu ratiba ya tenisi

"Cha kusikitisha zaidi ni kwamba bado vita vinaendelea, kwa hivyo bila shaka wachezaji wa Ukraine wana kila sababu ya kutotusalimia,” Kasatkina ameeleza.

"Nimekubali, na hivyo ndivyo ilivyo. Ni hali ya kusikitisha mno.”

Kasatkina amepangwa kucheza dhidi ya Veronika Kudermetova baadaye leo Jumatatu.