1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachimba mgodi 995 waliokwama Afrika Kusini waokolewa

Grace Kabogo
2 Februari 2018

Wachimba mgodi wote 955 waliokuwa wamekwama katika mgodi mmoja wa dhahabu nchini Afrika Kusini kwa zaidi ya saa 24 wameokolewa wakiwa salama. Wachimbaji hao walikwama baada ya umeme kukatika.

Südafrika, Unfall, Goldmine
Picha: Getty Images/G.Guercia

Wachimba mgodi wote 955 waliokuwa wamekwama katika mgodi mmoja wa dhahabu nchini Afrika Kusini kwa zaidi ya saa 24 wameokolewa wakiwa salama. Wachimbaji hao walikwama baada ya umeme kukatika.

Kampuni ya Sibanye Stillwater inayoumiliki mgodi huo wa Beatrix, ulioko katika jimbo la Free State, imesema leo kuwa wachimbaji wote watachunguzwa afya zao pamoja na kupatiwa huduma ya ushauri nasaha na kwamba wanatarajia mgodi huo kuanza kufanya kazi tena Jumatatu ijayo.

Msemaji wa kampuni hiyo, James Wellsted amesema kuwa baadhi ya wachimbaji hao wamepungukiwa maji mwilini na wengine wamechoka pamoja na kukabiliwa na shinikizo la damu, lakini hakuna mwenye hali mbaya wala walioko hatarini.

Mgodi wa SibanyePicha: Reuters/M. Hutchings

''Kwa hiyo shughuli zilisimama Jumatano jioni wakati umeme ulipokatika. Hatutaanza shughuli za uchimbaji kesho. Tunadhani wafanyakazi wetu wanahitaji muda wa kukaa na familia zao na bila shaka kupumzika. Tunapanga kuanza shughuli siku ya Jumatatu,'' alisema Wellsted.

Wellsted amesema mgodi huo unaopatikana kilomita 290, kusini magharibi mwa Johannesburg, una urefu wa mita 700 hadi 2,200 kwenda chini. Sababu za wachimbaji hao kukwama zinatokana na kukatika kwa umeme baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha dhoruba hali iliyozuia lifti kuwasafirisha wachimbaji kutoka chini ya ardhi. Baada ya saa kadhaa, wahandisi walifanikiwa kurejesha umeme na kuwapandisha juu wafanyakazi waliokuwa wamekwama tangu Jumatano jioni.

Wafanyakazi hao walipandishwa juu katika muda wa saa mbili. Mfanyakazi mmoja katika mgodi huo, Mike Khonto amesema hali ilikuwa ya kutisha kwani hapakuwa na hewa ya kutosha na wanaishukuru menejimenti ya kampuni yao kwa kuwapelekea chakula pamoja na maji.

Awali ndugu za wachimba mgodi hao walikusanyika katika barabara ya kuelekea kwenye mgodi, lakini walizuiwa na maafisa wa usalama wakati wakiendelea kusubiri taarifa kuhusu jamaa zao. Hata hivyo, chama cha wafanyakazi migodini nchini Afrika Kusini, NUM kimeelezea wasiwasi kwamba maisha ya wafanyakazi hao yamo hatarini na hapakuwa na mpango wa pili wa kuwaondoa wachimbaji hao.

Ndugu za wachimba mgodi wakiwasubiri jamaa zaoPicha: picture-alliance/AP

Chama hicho pia kimewataka wafanyakazi wa migodini kukataa kufanya kazi katika mazingira hatari na yasio salama na kimetaka kupatiwa majibu kutokana na tukio hilo. Nayo kamati ya bunge inayohusika na migodi imeelezea kusikitishwa na tukio hilo. Mwezi Agosti, wachimba migodi watano walikufa baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka nje kidogo ya jiji la Johannesburg.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zenye migodi mirefu zaidi ya dhahabu duniani. Dhahabu ni uti wa mgongo wa uchumi wa Afrika Kusini, lakini uzalishaji wake umeshuka kwa kiasi kikubwa kutokana na kupungua kwa vitalu vya dhahabu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga