1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachimba migodi waanza kuzikwa Uturuki

15 Mei 2014

Watu waliokufa kwenye ajali ya mgodi wa makaa ya mawe nchini Uturuki wameanza kuzikwa, huku idadi ya vifo ikiongezeka na vyama vya wafanyakazi vikiitisha maandamano ya kupinga usalama mdogo katika machimbo ya madini.

Mtu mmoja akiwa amekaa karibu na kaburi la ndugu yake aliyekufa kwenye ajali ya mgodi wa Soma.
Mtu mmoja akiwa amekaa karibu na kaburi la ndugu yake aliyekufa kwenye ajali ya mgodi wa Soma.Picha: Reuters

Ulitima. Unyonge na vilio. Maelfu ya waombolezaji wameyasindikiza majeneza yaliyobeba miili ya wachimba migodi hao katika miji na vijiji vya magharibi mwa nchi hiyo.

Miongoni mwa waliokumbwa na maafa hayo ni mapacha waliokuwa na umri wa miaka 32, Ismail Cata na Suleiman Cata, ambao wamezikwa kwenye kaburi moja kijijini kwao Manisa - ishara ya roho zilizozaliwa, kulelewa, kuishi na kufa pamoja.

Mwengine ni Kadir Ozer aliyekufa akiwa na umri wa miaka 33 na kuzikwa kwenye mji wa kwao wa Balikesir, ambapo Engin Yidrim mwenye umri wa miaka 40 alizikwa kwenye mji aliozaliwa wa Kutahya.

Jamaa wa Ozer wamewaambia waandishi wa habari kwamba ndugu yao alikuwa ameshastaafu kuchimba migodi, lakini akalazimika kurejea tena kazini ili apate kulipia mkopo wa nyumba yake.

Hatima ya wengine haijulikani

Bibi mmoja aliyepiga kambi nje ya mgodi huo wa Soma tangu usiku wa jana, amesikika akilia kwa uchungu wa kutokujua hatima ya mtoto wake.

Gari za kubebea wagonjwa zikiwa zimejipanga kusubiri kubeba maiti na majeruhi wa ajali ya mgodi wa Soma, kusini magharibi wa Uturuki.Picha: Getty Images

"Nina mjukuu wangu wa kiume huko chini, mkewe ni mja mzito na atajifungua ndani ya siku 17 kutoka leo," alisema bibi huyo.

Mjukuu wa bibi huyu ni kati ya wachimba migodi 150 ambao hadi sasa wamekwama umbali wa kilomita mbili chini ya ardhi, na ambao haifahamiki ikiwa bado wangali hai ama la. Waokowaji bado wanaendelea na kazi yao, lakini matumaini ya kuwapata watu wakiwa hai ni madogo.

Hadi sasa, serikali ya Uturuki imetangaza kwamba waliothibitika kufariki dunia kwenye ajali hiyo mbaya kabisa katika sekta ya madini, ni watu 282. Rais Abdullah Gul anatazamiwa kutembelea eneo la tukio hivi leo, umbali wa kilomita 480 kusini magahribi mwa mji wa Istanbul.

Maandamano ya wafanyakazi

Taarifa za awali zinaashiria kuwa mripuko kwenye mgodi huo ulisababishwa na hitilafu za umeme, lakini Mehmet Torun, mjumbe wa bodi ya mgodi huo na mkuu wa zamani wa Baraza la Wahandisi wa Migodini ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio, amesema makaa ya mawe yalipata moto na kusababisha kuvuja kwa hewa ya sumu kupitia mitaro ya mgodi huo.

Waandamanaji wanaopinga hali mbaya za kazi migodini wakikabiliana na askari wa kutuliza fujo mjini Istanbul.Picha: picture-alliance/dpa

Vyama vinne vya wafanyakazi vimeitisha mgomo wa siku moja wa kitaifa hivi leo kulalamikia hali mbaya ya usalama kwenye migodi nchini humo. Taarifa ya vyama hivyo imesema "Mamia ya kaka zetu huko Soma wamewachwa wafe tangu awali kabisa kwa kuwa walilazimishwa kufanya kazi katika hali ya kikatili sana ili kutengeza faida kubwa."

Kwa ujumla, rikodi ya usalama kwenye migodi ya makaa ya mawe nchini Uturuki imekuwa mbaya kwa miongo kadhaa sasa. Katika tukio kama hilo, hapo mwaka 1992, mripuko wa gesi uliuwa wafanyakazi 263 katika jimbo la Zonguldak, karibu na Bahari Nyeusi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW