1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachimba migodi waliokwama huko Chile wako hai

Kabogo Grace Patricia24 Agosti 2010

Wachimba migodi hao wamekwama tangu Agosti 5 baada ya mgodi waliokuwa wakifanyia kazi kuporomoka.

Rais wa Chile, Sebastian Pinera na Waziri wa Madini, Lourence Golbourne, wakishangilia taarifa za kuwepo hai wachimba migodi waliokwama.Picha: AP

Wachimba migodi 33 ambao wamekwama katika mgodi huko nchini Chile wamegundulika wakiwa hai na katika hali nzuri, wiki mbili baada ya kukwama katika shimo la mgodi, lakini wafanyakazi hao hawajaambiwa iwapo itachukua miezi kadhaa hadi hapo watakapoweza kuokolewa.

Wachimbaji hao ambao wanapatiwa chakula na madawa kupitia kwenye shimo dogo wamekwama katika eneo lenye urefu wa mita 700 chini ya ardhi, baada ya shimo la mgodi walilokuwa wakifanyia kazi kuporomoka. Taarifa za wachimbaji hao kuwa hai zimepokewa kwa furaha nchini Chile, ambako mwezi Februari mwaka huu ilikumbwa na tetemeko la ardhi lililowaua zaidi ya watu 500. Mhandisi anayehusika na zoezi la uokozi katika mgodi huo wa dhahabu wa San Jose pamoja na madini ya shaba, Andres Sougarett amesema alikuwa anaangalia eneo ambako wanaweza kuchimba shimo kubwa kwa ajili ya kuwatoa wachimbaji hao.

Hata hivyo, Sougarett amesema hajawaambia wachimba migodi hao muda halisi watakaotumia kuchimba shimo kwa ajili ya kuwaokoa, huku akikadiria kuwa inaweza ikachukua miezi mitatu hadi minne. Ajali hiyo katika mgodi huo imebadilisha taswira ya usalama wa migodini katika nchi ya Chile, ambayo ni ya kwanza katika kuchimba madini ya shaba duniani. Ajali ni nadra sana kutokea katika migodi mikubwa ya nchi hiyo. Wachimba migodi hao walipata mawasiliano na waokozi kupitia kifaa cha uchunguzi kilichowekwa katika mgodi huo.

Aidha, Waziri wa Madini wa Chile, Laurence Golborne amesema kuwa maafisa wa uokozi walianza kuwapelekea wachimba migodi hao mirija ya nailoni yenye maji ya kuwapatia nguvu mwilini yaani-glukosi pamoja na madawa ya kuzuia kupata vidonda vya tumbo, huku wahandisi wakiendelea na jitihada za kuchimba mashimo makubwa ya kuwaokoa. Hata hivyo, waziri huyo amesema wachimbaji hao wana njaa ikiwa ni siku ya 18 sasa wameishi bila chakula katika mgodi huo wenye joto na unyevunyevu. Kwa mujibu wa Waziri Golborne, wachimba migodi hao waliokwama tangu tarehe 5 ya mwezi huu wa Agosti, wameomba wapatiwe chakula na miswaki.

Mmoja wa wachimbaji hao waliokwama, Luis Urzua alimwambia Waziri Golborne kwa njia ya mawasiliano ya ndani kuwa wako salama na sasa wanasubiri kuokolewa. Katika ujumbe wao wamesema kuwa wamefanikiwa kuwa hai kwa kugawana vijiko viwili vya samaki aina ya tuna kila mmoja na nusu kikombe cha maziwa. Waziri wa Afya wa Chile, Jaime Manalich amesema kuwa wachimba migodi hao wanapatiwa vyakula vyenye protini nyingi na vya kutia nguvu ikiwemo aina fulani ya maziwa ya mgando, yaliyotengenezwa maalum kwa ajili ya wanaanga.

Katika hatua nyingine wamiliki wa mgodi huo wamesema janga hilo limeiweka kampuni yao katika hatari ya kufilisika na kwamba wanaweza wakashindwa kuwalipa wachimba migodi hao watakapookolewa. Hadi siku ya Jumapili hakukuwa na mawasiliano yoyote na wachimba migodi hao na matumaini ya kupatikana wakiwa hai yalikuwa yamefifia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW