Wachimba migodi haramu 14 wakamatwa Afrika Kusini
25 Novemba 2024Kundi hilo la wanaume 14 liliibuka lenyewe kutoka kwenye mgodi wa bafflesfontein usiku wa kuamkia leo wakati operesheni ya kuifunga migodi haramu ya madini ikiendelea nchi nzima.
Msemaji wa polisi Athlenda Mathe anasema kuwa mvulana wa miaka 14 alikuwa miongoni mwa wanaume waliojitokeza na amethibitisha kile ambacho polisi wamekuwa wakikisema kuwa, ndani ya mgodi huo kuna silaha nzito za wachimbaji haramu.
"Wanathibitisha kile ambacho tumekuwa tukisema kwamba kuna wachimbaji haramu huko chini wenye silaha nzito, kwa hivyo tunataka tu kuonyesha kwamba upelelezi wetu iko imara." amesema Afisa huyo.
Mathe anasema wamefahamishwa kuwa watu wenye silaha wamekuwa wakiwashikilia mateka wachimbaji wengine haramu chini ya ardhi.
"Wanatuambia pia kwamba chakula na maji ambayo yanatumwa mgodini yanachukuliwa na watu hawa wenye silaha nzito na hawawapi wachimbaji wengine, wanatumia wenyewe kwa sababu wanataka kuendelea na shughuli zao za uchimbaji haramu."
Operesheni hiyo ya kuwatoa kwa nguvu wachimba migodi haramu yagharimu randi milioni 1
Katika awamu ya kwanza ya operesheni ya uokoaji, kifusi karibu na shimo la kuingia mgodini humo kiliondolewa, na awamu ya pili, ambayo ilianza Ijumaa iliyopita, ilishuhudia mashine za kunyanyua vitu vizito zinazotumiwa viwandani zikiingiza kamera mgodini kama sehemu ya tathmini ya kile kinachoendelea mgodini.
Operesheni hiyo inayogharimu randi milioni 1 kwa siku inasemekana kuwa ya kwanza na ya aina yake nchini humo.
Kwa upande mwingine Bazilio Zenobi, mwanaharakati wa kutetea haki za wachimba migodi na mfanyabiashara wa madini amesema kitendo cha huduma kukatwa kwa wachimbaji haramu si cha kiungwana.
Matukio ya hivi karibuni ya kuibuliwa kwa wachimba migodi haramu yamejiri kufuatia operesheni katika mgodi wa Vala uliopo hapa kaskazini magaribi mwa Afrika Kusini ambapo zaidi ya wachimba migodi haramu 1,000 walikamatwa wiki chache zilizopita.
Mamia ya wachimba migodi haramu wanaaminika bado wamekwama chini ya ardhi kwenye shimo lenye kina cha zaidi ya kilomita 2.
Asasi za kiraia zinaowawakilisha wale waliobaki katika machimbo ya Stilfontein hapa Kaskazini Magharibi zimesema kwamba, wachimbaji hao wako tayari kutoka, lakini operesheni za polisi zinawaogopesha.