1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Wachimbamadini 41 wauawa katika mripuko mgodini Uturuki

Daniel Gakuba
15 Oktoba 2022

Mripuko kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Bartin kaskazini mwa Uturuki umewauwa watu 41, na shughuli za uokozi zinaendelea kuwatafuta walionaswa ndani ya mgodi. Gesi ya metani inaelezwa kuwa chanzo cha mripuko huo.

Türkei | Grubenunglück in Bartin
Shughuili za uokozi kwenye eneo la mgodi uliokumbwa na mripukoPicha: Gokhan Yilmaz/AA/picture alliance

Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Suleyman Soylu amesema wakati wa mripuko, watu 110 walikuwa ndani ya mgodi huo, na kwamba 58 miongoni mwao walikuwa tayari wameokolewa wakiwa salama.

''Bado moto unawaka mgodini, wachimbaji pamoja na waokoaji wamejitolea pakubwa kuhakikisha hakuna ndugu yao anayeachwa nyuma,'' amesema waziri Soylu ambaye amekwenda kwenye eneo la ajali, na kuongeza kuwa bado mchimbaji mmoja hajulikani alipo.

Soma zaidi: Wachimbaji waliookolewa baada ya siku 41

Picha za televisheni zimeonyesha makundi ya watu waliojawa na simanzi, baadhi wakibubujikwa na machozi, nje ya lango kuu la kuingia kwenye mgodi, wakisubiri kupata taarifa juu ya majaliwa ya wapendwa wao waliokuwa mgodini.

Jamaa wa wachimbamigodi walionaswa migodini wakisubiri kwa shauku kujua hali ya wapendwa waoPicha: AYHAN ACAR-BARTIN/DHA

Habari za mwanzo kuhusu walionaswa mgodini zilitolewa na wenzao walioweza kukimbia haraka na kutoka nje. Meya wa wilaya ya Amsara ulipo mgodi ulioathirika, Recai Cakir amesema wengi wa walionusurika mkasa huu wamepata majeraha mabaya.

Erdogan njiani kuelekea eneo la ajali

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitarajiwa kusafiri kwa ndege kuzuru eneo la ajali hiyo, na kupitia ukurasa wake wa twitter aliapa kuwa uchunguzi wa kina utafanyika kubainisha kilichotokea.

Waziri wa nishati Fatih Donmez alidokeza baadaye kuwa kwa sehemu kubwa moto uliozuka mgodini hapo ulikuwa umedhibitiwa, huku juhudi za kupoza eneo ulipotokea moto huo, kiasi cha mita 350 chini ya ardhi, zikiendelea.

Soma zaidi: Watu 14 wafariki Congo baada ya mgodi kuporomoka

Meya wa Amsara, Recai Cakir mesema wafanyakazi wa uokozi wapatao 70 walikuwa wameweza kufika kwenye chanzo cha mripuko, katika kina cha mita zipatazo 250 chini ya ardhi.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitarajiwa kuuzuru mgodi uliokumbwa na maafaPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Kulingana na waziri wa mambo ya ndani, Suleyman Soylu, wachimbamigodi 10 wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za Bartin na Istanbul, na mmoja tayari ameruhusiwa kurudi nyumbani.

Gesi ya metani ndio chanzo cha mripuko

Duru za serikali ya Uturuki zimeeleza kuwa waendeshamashtaka wameanzisha uchunguzi kujua chanzo cha moto huo. Taarifa za mwanzo hata hivyo zinaashiria kuwa gesi ya metani mgodini ndio imeuanzisha moto huo.

Soma zaidi: Wachimba mgodi 955 waliokwama Afrika Kusini waokolewa

Awali, shirikisho la huduma za kushughulikia majanga nchini Uturuki, AFAD lilikuwa limearifu kuwa moto umeanzishwa na cheche kwenye transfoma iliyokumbwa na hitilafu, lakini baadaye limeiondoa dhana hiyo, likiafikiana na ile ya mrundikano wa gesi ya metani.

Mwaka 2014, wafanyakazi 301 waliuawa katika ajali mbaya kabisa ya mgodini nchini Uturuki, katika mji wa Soma ulio umbali wa kilomita 350 kusini mwa Istanbul.

Vyanzo: rtre, afpe

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW