1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachunguzi wa silaha za kemikali washindwa kuingia Syria

Sylvia Mwehozi
20 Aprili 2018

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa amesema Urusi na Syria zinapaswa kuzingatia ahadi waliyotoa ya kuwaruhusu wachunguzi wa silaha za kemikali kutembelea eneo linaloshukiwa kufanyika shambulio la gesi ya sumu.

Syrien Ost-Ghuta leere Raketenhülse
Picha: Getty Images/AFP/H. Mohamed

Karen Pierce amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press kwamba "ni muhimu sana  kuliko wakati wowote kuruhusu timu, kuisindikiza, kuhakikisha iko salama na kuhakikisha kwamba itafanya kazi yake".

Timu ya usalama ya Umoja wa Mataifa ambayo ilipaswa kuwasafishia njia wachunguzi kutembelea eneo hilo, ilishambuliwa wakati ikitembea eneo linalodaiwa kushambuliwa mjini Douma siku ya Jumanne. Ziara hiyo imesitishwa na Umoja wa Mataifa unasema timu ya usalama inapaswa kurejea ili kuangalia hatua za usalama kabla ya tume ya kufuatilia ukweli kutoka shirika linalozuia silaha za kemikali haijakwenda mjini Douma. 

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Karen PiercePicha: picture-alliance/AA/M. Elshamy

"Waziri Mkuu amekuwa wazi kwamba tunataka wachunguzi hao waingie na kutafuta ukweli sahihi na tutaendelea kutumia nyenzo za kisiasa na kiuchumi kwa Wasyria, kuwashawishi kushirikiana na taratibu za kimataifa na kuharibu mpango wa silaha za kemikali zisizo halali, amesema Pierce.

Wafuatiliaji wa kwanza na wanaharakati wanasema zaidi ya watu 40 waliuawa katika shambulio la Aprili  7, wengi walikutwa na povu kwenye midomo ishara ya kukosa hewa. Urusi imesema silaha za kemikali hazikutumika mjini Douma na hivi karibuni iliwatuhumu waasi kwa kupanga shambulio hilo kushirikiana na Uingereza, madai ambayo Pierce na maafisa wa Uingereza wanayakataa vikali.

Marekani, Ufaransa na Uingereza zilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vinavyodhaniwa kuzalisha silaha za kemikali vya serikali ya Syria baada ya kuhitimisha kwamba majeshi ya rais Bashar al Asaad yalitekeleza shambulio hilo, ingawa madai yao hawajadhibitisha hadharani.

Picha inayoonyesha majengo yaliyoharibiwa mjini DoumaPicha: Getty Images/AFP

Hayo yakiendelea jeshi la Syria limeshambulia kwa mabomu wanajihadi katika eneo la mwisho nje ya udhibiti wa serikali karibu na mji wa Damascus usiku wa kuamkia leo, wakati rais Bashar al Assad akiendeleza jitihada zake za kuyatwaa maeneo yote yaliyosalia.

Mashambulizi ya anga ya Marekani, Ufaransa na Uingereza siku ya Jumamosi ya kumuadhibu Assad hayajabadili lolote kupunguza kasi ya vikosi vyake, hivi sasa wakiwa katika nafasi nzuri kuanzia kwenye vita ya miaka saba.

Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria limesema, mashambulizi ya anga yamefanyika dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Kipalestina ya Yarmouk pamoja na eneo la al-Hajar al-Aswad, sehemu ndogo ya eneo la waasi lililogawika baina ya wanajihadi wanaopigana na waasi wengine walio kusini mwa mji mkuu.

Na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kuwasili hii leo nchini Sweden katika mkutano usio rasmi na katibu mkuu Antonio Guterres, wakiwemo pia mabalozi wa Marekani na Syria katika Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW