1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wacongo wapiga kura kumchagua rais mpya

30 Desemba 2018

Raia wa DRC wanapigakura Jumapili hii katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kupelekea mabadilishano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960.

Kongo vor der Wahl
Afisa wa uchaguzi akibandika orodha ya wapigakura katika kituo cha kupigia kura cha Katendere mjini Goma, Desemba 29, 2018.Picha: Getty Images/AFP/P. Meinhardt

Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwa madarakani tangu kuuawa kwa baba yake mnamo mwaka 2001, ataachia ngazi katika hatua ya kihistoria kwa taifa ambalo limeshuhudia utawala wa kiimla, mapinduzi ya kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu lilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Kukubali kwake kuheshimu ukomo wa mihula kunawakilisha hatua mbele kwa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini. Wakosoaji hata hivyo, wanasema huenda uchaguzi huo ukakumbwa na udanganyifu, na kwamba Kabila huenda akaendelea kutawala kupitia nyuma ya pazia. Hajaondoa uwezekano wa kuwania tena urais mwaka 2023.

Licha ya kuahirishwa mara kwa mara kwa uchaguzi huo ambao awali ulipaswa kufanyika mwaka 2016, wanadiploamsia na waangalizi wa uchaguzi wanasema serikali haijafanya maandalizi ya kutosha, na kuibua wasiwasi wa kurudiwa kwa vurugu zilizofuatia uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011.

Vikosi vya usalama vimeua zaidi ya nusu dazeni ya wafuasi wa upinzani kwenye kampeni na maandamano ya vurugu yaliripuka wiki hii baada ya maafisa kutangaza kuwa ngome tatu za upinzani, zinazochangia wapigakura milioni 1.2 kati ya jumla ya wapigakura milioni 40 nchini kote, hazitaweza kushiriki uchaguzi kutokana na hatari za kiafya zinazosababishwa na mripuko unaoendelea wa Ebola na vurugu za kikabila.

Wanadiplomasia wa kigeni waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba karibu asilimia 60 tu ya vifaa vya kupigia kura vilikuwa vimewasilishwa nchini kote, na waangalizi wa uchaguzi wamesema vituo vya kupigia kura katika mji mkuu Kinshasa vitapambana kuwahudumia wapigakura wote wakati wa muda wa kupiga kura, unaoanza saa 12 asubuhi hadi saa 11 jioni.

Wapinzani wahofia wizi wa kura

Wapinzani wa Rais Kabila wanasema serikali inajaribu kupindua matokeo ya uchaguzi kumpa ushindi mrithi wake anaempendelea, waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary, ambaye uchunguzi wa maoni ya wapigakura unamuonyesha akiwa nyuma ya wagombea wawili wa upinzani.

Matokeo ya uchunguzi wa karibuni zaidi yaliotolewa na idara ya utafiti wa Congo ya chuo kikuu cha New York siku ya Ijumaa, yalionyesha kuwa meneja wa zamani wa kampuni ya Exxon Mobil na mbunge wa upinzani Martin Fayulu anaongoza kwa asilimia 47. Mgombea mwingine wa upinzani, Felix Tshikedi alikuwa akifuatia kwa asilimia 24, huku Shadary akiwa na asilimia 19.

Mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary (juu kushoto), kiongozi wa upinzani Vital Kamerhe (juu kulia), kiongozi wa chama cha UDPS Felix Tshisekedi (chini kushoto) na Martin Fayulu, mgombea wa muungano wa upinzani (chini kulia).

Fayulu na Tshisekedi wamezungumza kwa kujiamini kuhusu ushindi, lakini Shadary ana faida kubwa ya kitaasisi, ikiwemo kupewa nafasi kubwa katika vyombo vya habari vya serikali. Wateule wa Kabila pia wanadhibiti taasisi nyingi za kitaifa. "Kesho nitakuwa rais," Shadary aliliambia shirika la habari la reuters kwa njia ya simu.

Wapinzani wake wanautuhumu muungano unaotawala kwa kuandaa mazingira ya wizi wa moja kwa moja wa kura, ambapo wasiwasi wao kwa sehemu kubwa umejikita kwenye mashine za kupigia kura zisizowahi kujaribiwa, ambazo zinatumiwa katika uchaguzi kwa mara ya kwanza.

Tume ya Taifa ya uchaguzi (CENI) imejaribu kuwahakikishia wapinzani kwamba karatasi tu zilizochapishwa kutoka kwenye mashine hizo ndiyo zitahesabiwa katika matokeo rasmi.

Lakini mgogoro wowote unaweza kusababisha mporomoko mkubwa wa kiusalama nchini Congo, hasa kwenye mipaka yake na Rwanda, Uganda na Burundi, ambako dazeni kadhaa za makundi ya wapiganaji wako mashughuli.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Yusra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW