1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wademocrat wachungulia udhibiti wa Seneti Marekani

6 Januari 2021

Mgombea chama cha Democratic ameshinda kiti kimojawapo cha uwakilishi wa baraza la seneti, huku mgombea mwingine wa Democratic akiongoza kwa kura chache wakati kura za mwisho zikihesabiwa katika jimbo hilo la kusini.

USA Georgia | Senatswahl: Raphael Warnock
Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Ni suala lenye umuhimu mkubwa kwa ajenda ya utungaji sheria ya rais mteule Joe Biden. Ikiwa Wademocrat wote wawili watashinda, baraza la seneti litagawanyika kwa wajumbe 50 kwa 50 ambapo makamu wa rais Kamala Harris atakuwa mwenye kura ya maamuzi.

Soma pia:Biden aongoza katika majimbo muhimu, Georgia na Pennsylvania

Mgombea wa Democratic Raphael Warnock ametangazwa na vituo kadhaa vya utangazaji vya Marekani kuwa mshindi wa kinyang'anyiro chake dhidi ya Seneta wa sasa, Mrepublican Kelly Loeffler.

Mgombea wa pili wa seneti Jon Ossoff, pia amejitangazia ushindi. Ikiwa atathibitishwa, Wademocrat na Warepublican watakuwa na wawakilishi 50-50 na kumpa makamu wa rais Kamala Harris kura ya maamuzi.Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Warnock, mwanagenzi kwenye siasa mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni mchungaji wa kanisa la Atlanta ambako kiongozi wa vuguvugu la haki za kiraia Martin Luther King Jr alihubiri, alikuwa na uongozi wa asilimia moja baada ya karibu kura zote kuhesabiwa. Warnock atakuwa mtu wa kwanza mweusi kuiwakilisha Georgia katika baraza la seneti.

"Georgia, nimefarijika na imani mlioonesha kwangu. Na nawaahidi usiku huu: Nakwenda kwenye seneti kufanya kazi kwa ajili ya wakazi wote wa Georgia, bila kujali nani mliempigia kura katika uchaguzi huu," alisema Warnock baada ya mashirika ya habari kumtangaza mshindi.

Soma pia:Biden apata kura zaidi Georgia na kumpiku Trump

Machungu yaongezeka kwa rais Trump

Katika kinyang'anyiro kingine cha Jumanne, Jon Ossoff, mkuu wa zamani wa kampuni ya filamu za makala mwenye umri wa miaka 33, alikuwa na uongozi mwembamba dhidi ya mgombea wa Republican David Perdue mwenye umri wa miaka 70. Kukiwa bado kumesalia kura elfu kadhaa, vyombo vya habari vya Marekani vilikuwa havijatangaza mshindi wa mchuano huo.

Ushindi wa Wademocrat jimboni Georgia utaimarisha nafasi ya rais mteule Joe Biden katika kupitisha ajenga yake bila vizuizi vya Warepublican.Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Ikiwa Warepublican watapoteza kinyang'anyiro hicho cha pili, litakuwa janga la kisiasa, saa chache tu kabla ya rais Donald Trumpkupata pigo jengine chungu wakati bunge litakapothibitisha ushindi wa Biden katika kura ya jopo maalumu la wajumbe wa majimbo.

Soma pia:Trump asikika akimtaka afisa wa uchaguzi 'kumtafutia kura'

Warepublican kadhaa wameashiria watazwia kura hiyo ya kuthibitisha ushindi. Lakini idadi yao inaonekana ndogo sana na mabaraza ya wawakilishi na seneti yana uhakika kukataa juhudi hizo na kuthibitisha matokeo ya kura ya wajumbe wa majimbo.

Chanzo: Mashirika